Vitendo vya kigaidi vinabomoa na wala havijengi kamwe!
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Chama cha Waisraeli wa Argentina kinachoadhimisha
miaka ishirini tangu shambulizi la kigaidi lilipofanywa dhidi ya makao makuu ya chama
hiki kunako tarehe 18 Julai 1994 anasema kwamba, vitendo vya kigaidi vinabomoa, havijengi
wala kusaidia maendeleo ya binadamu. Katika shambulio hilo watu 85 walipoteza maisha
na wengine 200 kupata majeraha makubwa.
Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuonesha
mshikamano wake wa dhati na Jumuiya ya Waisraeli wa Argentina pamoja na wale wote
walioguswa na madhara ya shambulio hili la kigaidi. Baba Mtakatifu anakumbuka kwa
uchungu mkubwa jinsi ambavyo vitendo hivi vimekatisha maisha ya watu wasiokuwa na
hatia; vimeharibu matumaini ya watu na kwamba, Buenos Aires inapaswa kuwalilia watoto
wake kwa uchungu mkubwa. Matukio kama haya hayapaswi kusahaulika haraka kiasi hiki,
kwani historia inapaswaiwasaidie watu kuboresha mahusiano yao ya kijamii.
Baba
Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, haki inatendeka. Baba Mtakatifu
anahitimisha ujumbe wake kwa sala kwa ajili ya kuziombea roho za marehemu waliofariki
dunia katika tukio hili pamoja na familia zao.