2014-07-19 09:56:01

Ninakutumainia!


Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, LEV, kimechapisha kitabu kinachotoa maelezo ya kina, mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Majandokasisi na Wanovisi wanaojiandaa kwa ajili ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Jirani zao. Kitabu hiki ambacho kinaitwa "Ninakutumainia" kinakazia kwanza kabisa: ukweli, uwazi na udumifu kama kanuni msingi kwa vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya kumtumikia Mungu kama Mapadre na Watawa.

Kitabu hiki ni matunda ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kuadhimishwa kwa kishindo kikuu na Papa Francisko. Itakumbukwa kwamba, tarehe 4 hadi tarehe 7 Julai 2013, Mji wa Roma ulikuwa umefunikwa kwa uwepo wa makundi ya vijana yaliyokuwa yanaadhimisha Mwaka wa Imani. Mang'amuzi, ushuhuda na changamoto zilizotolewa wakati huo, zimekusanywa na kuhaririwa na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya.

Kitabu hiki kina mahubiri na tafakari zilizotolewa na Baba Mtakatifu alipokutana na vijana hawa pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Shuhuda mbali mbali zilizotolewa na vijana hawa zimepamba kitabu hiki ambacho kwa sasa kinapatikana kwenye maduka ya vitabu mjini Roma.

Utangulizi wa kitabu hiki umetolewa na Askofu mkuu Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anayekazia umuhimu wa ushuhuda kama kanuni msingi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Vijana wanahamasishwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake pasi na kujibakiza hata kidogo, kwa kutambua kwamba, maamuzi haya magumu yanawawajibisha.

Kitabu hiki kinafungwa kwa tafakari ya kina inayotolewa na Kardinali Angelo Comastri pamoja na kupambwa kwa picha za vijana wengi waliohudhuria katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.