2014-07-19 15:04:02

Mwaliko kwa Waamini kutoka Korea ya Kaskazini kushiriki katika Ibada wakati wa hija ya Papa Francisko nchini Korea


Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, limetuma mwaliko kwa Jumuiya ya Waamini Wakatoliki kutoka Korea ya Kaskazini kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Korea kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 18 Agosti 2014. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ya kichungaji sanjari na siku ya sita ya vijana Barani Asia ni“Ondoka, uangaze kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia”

Ujumbe wa viongozi wa Kanisa Katoliki Korea ya Kusini katika siku za hivi karibuni wamekutana na kuzungumza pamoja na kutoa ujumbe wa amani kati ya wananchi wa Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini. Mwaliko huu umepokelewa kwa mikono miwili, lakini itawabidi waamini kutoka Korea ya Kaskazini kufanya tafakari ya kina kabla ya kuchukua maamuzi.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Andres Yeom Soo-jung, hivi karibuni kwa mara ya kwanza, alitembelea Korea ya Kaskazini ili kukutana na waamini wa Kanisa Katoliki wanaofanya kazi viwandani, Korea ya Kaskazini. Kardinali Andres ameonesha matumaini yake kwamba, majadiliano baina ya pande hizi mbili, hatimaye, siku moja yatasaidia kuleta amani.

Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Korea kunako mwaka 1984 na kurudi tena nchini humo mwaka 1989. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa pili kutembelea tena Korea.








All the contents on this site are copyrighted ©.