2014-07-19 08:44:29

Jimbo Katoliki Daejeon, Korea ya Kusini ni chemchemi ya mashahidi wa imani


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Korea katika maadhimisho ya Siku ya sita ya Vijana Barani Asia inayoongozwa na kauli mbiu “Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia” atapata nafasi ya kuonja ukarimu kutoka kwa waamini wa Jimbo Katoliki la Daejeon, lililoko Korea ya Kusini, mahali ambako si maarufu sana kwa wengi, lakini hapa ndipo ambapo Baba Mtakatifu Francisko amepaona na kuamua kupatembelea. RealAudioMP3

Askofu Lazaro You Heung-sik wa Jimbo Katoliki Daejeon anasema mashahidi wengi wa Korea waliojisadaka kwa ajili ya kushuhudia Injili wanatoka katika Jimbo hili. Anakumbuka alipokutana na kuzungumza na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1981 na kumwahidia kwamba, atajitahidi kuwa Padre mwema kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kanisa la Kristo, jambo ambalo lilimvutia Papa Yohane Paulo II ambaye alimzawadia Rozari tatu na baadaye katika ujumbe wake kwa Mapadre kwa mwaka ule, aliwataka Makleri kuwa kweli ni mfano wa kuigwa.

Askofu Lazaro You Heung-sik anasema, katika barua aliyomwandikia Baba Mtakatifu Francisko akimwomba kushiriki katika Kongamano la sita la Vijana Barani Asia alimwelezea umuhimu wa Jimbo lake katika mchakato wa ushuhuda wa maisha miongoni mwa waamini kwani hapa ni kisima na chemchemi ya maisha ya mashahidi wengi waliojisadaka kwa ajili ya kusimamia kweli za Kiinjili. Hapa ni mahali ambapo, waamini walei wamejijenga na kujiimarisha katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo mjini Yerusalemu.

Waamini wa Jimbo Katoliki Daejeon wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii aliyowakirimia, ili kumwonjesha Baba Mtakatifu ukarimu na ushuhuda wa maisha ya waamini kutoka Korea. Kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 17 Jimbo hili litakuwa ni mwenyeji wa Siku ya Vijana Korea sanjari na Siku ya Vijana Barani Asia, Itakumbukwa kwamba, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani mwaka 2013 iliyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil, Korea iliwakilishwa na kundi la vijana 350, hawa kweli wameendelea kuwa ni Wamissionari miongoni mwa vijana wenzao. Wako tayari kutoka kimasomaso bila woga wala makunyanzi kwa ajili ya kuhudumia.

Waamini na watu wenye mapenzi mema, walishangazwa sana kusikia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko wa kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya sita ya Vijana Barani Asia, tukio ambalo kwa hakika litaacha kumbu kumbu ya kudumu katika mioyo ya vijana, waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Korea. Huu ni mwaliko na changamoto ya kuendeleza pia majadiliano ya kidini na kiekumene na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Korea na Asia katika ujumla wake, ili haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu miongoni mwa waamini uweze kutawala na kudumishwa.

Ukristo nchini Korea ni matunda ya Mmissionari kutoka Asia aliyefika nchini humo kunako mwaka 1794 na kukuta kwamba, kuna waamini elfu nne waliokuwa wamebatizwa. Kufumuka kwa vita kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini kati ya mwaka 1950 hadi mwaka 1953 kulisababisha madhulumu makubwa dhidi ya Wakristo kiasi kwamba, watu wengi wakakata tamaa kutokana na vita pamoja na madhara yake ambayo bado yanaendelea kuwatendea vibaya wananchi wa Korea zote mbili.

Maadhimisho ya Siku ya sita Barani Asia yatakuwa ni jukwaa la Uinjilishaji, fursa ya majadiliano ya kina na Baba Mtakatifu Francisko kwa heshima ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni, Mama wa Kristo na Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.