Sala kwa ajili ya kuombea amani Cameroon na maeneo yanayobaliwa na vita!
Askofu mkuu Samuel Kleda wa Jimbo kuu la Douala nchini Cameroon, ambaye pia ni Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon anasema, Jumamosi, tarehe 19 Julai 2014 ni
siku ya kuombea amani nchini Cameroon na maeneo ambayo yanakabiliwa na vita kwa wakati
huu. Kanisa linapenda kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini
Cameroon kutambua hatari kubwa iliyoko mbele yao inayofichika katika mashambulizi
ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram kutoka Nigeria, kwenye maeneo yaliyoko
Kaskazini mwa Cameroon.
Jumamosi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema
wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kufanya maandamano kwa ajili ya kuombea amani,
utulivu na ustawi nchini Cameroon pamoja na kuomba tunza na ulinzi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yanayotishia usalama wa watu na mali zao. Mashambulizi
haya ni tishio kwa mshikamano wa kitaifa kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo,
kumbe kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja, ili kupinga na kudhibiti vitendo vya kigaidi
vinavyofanywa na Boko Haram.