Papa azungumza kwa njia ya simu na Rais Peres na Rais Abbas!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa asubuhi tarehe 18 Julai 2014 amempigia simu Rais
Peres Shimon wa Israeli na Mahmoud Abbas wa Palestina ili kuwaelezea masikitiko yake
makubwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea kwenye Ukanda wa Ghaza, hali ambayo
inachochea na kuendeleza uhasama kati ya wananchi wa mataifa haya mawili pamoja na
kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kutokana na mashambulizi hayo, watu
wengi wanateseka sana na kwamba, wanahitaji msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.
Mazungumzo
ya simu kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Marais wa Israeli na Palestina ni mwendelezo
wa juhudi zake za makusudi kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati kama
alivyofanya, Jumapili tarehe 13 Julai 2014 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Baba
Mtakatifu bado anakumbuka moyoni mwake, hija yake ya kichungaji aliyoifanya Nchi Takatifu
pamoja na ule mkutano kwa ajili ya kuombea amani Mashariki ya Kati, uliowakutanisha
viongozi kutoka Israeli na Palestina mjini Vatican hapo tarehe 8 Juni 2014.
Katika
mazungumzo yake, Baba Mtakatifu amewahakikishia Marais hawa sala za Kanisa kutoka
sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuombea amani katika Nchi Takatifu. Hawa
ni watu wa amani, wanataka amani na wataendelea kuombea amani hadi pale amani ya kweli
itakapopatikana huko Mashariki ya Kati.
Amewakumbusha viongozi wa kitaifa
na kimataifa kwamba, wanadhamana nyeti ya kulinda na kudumisha amani kwa kusitisha
chuki, kinzani na uhasama kati ya Waisraeli na Wapalestina, ili kutoa fursa kwa mchakato
utakaositisha vita, ili amani na upatanisho vianze tena kuchipuka kutoka katika mioyo
ya watu!