Tume ya Afrika ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, imeidhinisha kiasi
cha dolla za Kimarekani millioni 1. 3 kwa ajili ya kugharimia miradi arobaini na sita
kwa ajili ya Kanisa Barani Afrika. Maamuzi haya yamefanywa na Maaskofu Katoliki Marekani
katika mkutano wao uliofanyika hivi karibuni huko New Orleans.
Kanisa Barani
Afrika linaendelea kukua na kupanuka kwa kasi ya ajabu na kwamba linakabiliwa na changamoto
mbali mbali katika kuzima kiu ya maendeleo ya watu wanaowazunguka, anasema Kardinali
Theodore McCarrick, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Washington DC, ambaye kwa
sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.
Msaada
huu unalenga kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kuweza kuandaa rasilimali watu ili kutekeleza
kazi ya Uinjilishaji mpya kwa kuwa na utaalam na ujuzi unaohitajika ili kuongeza tija
na ubora wa shughuli za kichungaji. Pili ni kuendelea kulisaidia Kanisa Barani Afrika
kujenga uwezo ili hatimaye, liweze kujitegemea na kujiendesha lenyewe kwa kutumia
kikamilifu rasilimali watu na vitu vilivyoko Barani Afrika kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Bara la Afrika na watu wake kwa ujumla. Hapa kuna haja ya kuwaandaa viongozi
wanaoweza kujisadaka na kujitosa kwa ajili ya Kanisa la Bara la Afrika.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Marekani litaendelea kushirikiana na Kanisa Barani Afrika ili
kufikia malengo yaliyobainishwa na pande hizi mbili. Taarifa zinaonesha kwamba, Baraza
la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, limepewa msaada wa dolla za kimarekani 30,
000 ili kusaidia majiundo makini ya viongozi, gharama za uendeshaji pamoja na mikakati
ya haki na amani. Wanawake kutoka Afrika ya Kusini, Bostwana na Swaziland wanatarajiwa
kunufaika na msaada huu.
Kiasi cha dolla za kimarekani 25, 000 zimetolewa kwa
Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha utekelezaji
wa Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha, “Evangelii
gaudium” katika lugha ya taifa. Fedha hii itagharimia mafunzo kwa viongozi wa kitaifa
ambao baadaye watashirikisha mang’amuzi yao katika ngazi za Kijimbo na Kiparokia.
Kardinali
Theodore McCarrick anasema, msaada unaotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani
unalenga kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kutekeleza utume wake hasa miongoni mwa
Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, changamoto inayotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko. Msaada unaotolewa kwa Kanisa Barani Afrika ni sehemu ya Mfuko
wa mshikamano kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.