2014-07-18 12:07:05

Malawi kuendeleza mchakato wa haki, amani na uhuru wa kuabudu!


Serikali ya Malawi itaendeleza mchakato wa waamini wa dini mbali mbali kuishi kwa amani na utulivu nchini humo licha ya tofauti zao za kiimani na kidini. Ni changamoto kwa viongozi wa kidini kusaidia kupambana na malimwengu, kwa kuwapatia waamini kanuni maadili na tunu msingi za maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Ni changamoto iliyotolewa na Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi wakati alipokuwa anawahutubia wajumbe wa Mkutano wa kumi na nane wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya mkutano huo, Alhamisi, tarehe 17 Julai 2014.

Rais Mutharika amelipongeza Kanisa Katoliki kwa huduma makini linayotoa kwa wananchi wa Malawi na Afrika Mashariki katika ujumla wake, hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya yaani Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo, imekuja kwa wakati muafaka kwani wakati huu, watu wengi wanaendelea kumezwa na malimwengu pamoja na nguvu za giza. Kuna athari kubwa za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia Barani Afrika; mambo yanayoathiri maisha na utamaduni wa watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.