2014-07-18 10:41:47

Jisikieni wamoja ndani ya Kristo!


Ilikuwa ni tarehe 21 Novemba 1964 Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa VI alipotia mkwaju Waraka wa Kichungaji kuhusu Majadiliano ya Kiekumene "Unitatis Redintegratio", matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kama sehemu ya maandalizi ya tukio hili muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, limewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Ujumbe wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya mchakato wa Umoja wa Wakristo.

Maaskofu wanasema umoja miongoni mwa Wakristo ni changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi na Wakristo wote, kwani hili ni agizo la Kristo mwenyewe ili wote wawe wamoja. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, Kanisa limepiga hatua kubwa ya majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kikristo, hii ni njia iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Wakristo wamepiga hatua kubwa kwa kufahamiana na kushirikiana kwa pamoja kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Ni katika mchakato huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, kunako mwaka 1965 likaanzisha Tume ya Majadiliano ya Kiekumene na Kidini. Malengo makuu ya tume yalikuwa ni kuanzisha mahusiano na Makanisa ya Kikristo nchini Canada; kuwa ni mahali pa kufanya rejea katika mikakati ya majadiliano ya kidini na kiekuemene pamoja na kuhamasisha majadiliano ya kiekumene katika ngazi ya ktaifa.

Kunako mwaka 1998, Tume hii ikawa na hadhi ya Baraza la Kiekumene kama yalivyo kwa Makanisa mengine nchini Canada. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika kukuza na kudumisha mahusiano ya kiekumene kati ya Makanisa ya Kikristo. Ni mahusiano yanayojikita katika maisha ya: Sala, ushuhuda na ukarimu wa wafuasi wa Kristo.

Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Majadiliano ya Kiekumene, iwe ni fursa kwa Wakristo kushikamana zaidi kwa kuwa wamoja ndani ya Kristo sanjari na kuendelea kupandikiza mbegu ya imani, unyenyekevu, uvumilivu, toba na msamaha ili kuponya madonda ya utengano yaliyojitokeza ndani ya Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kwa namna ya pekee, linakumbuka tukio la kihistoria lililowakutanisha Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli mjini Yerusalemu wakati wa kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa Paulo wa VI na Patriaki Anathegoras walipokutana kusali pamoja. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawahimiza waamini kama mtu binafsi na Jumuiya kujikita katika kuhamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, kwa kuanzia katika familia, shule na Parokia mbali mbali! Wakristo wote wajisikie kuwa wamoja ndani ya Kristo!







All the contents on this site are copyrighted ©.