AMECEA wasikitishwa na ukosefu wa uhuru wa kidini kwa baadhi ya nchi!
Askofu mkuu Tarcisio Ziyaye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika hotuba yake ya kuwakaribisha wajumbe wa AMECEA,
Alhamisi, tarehe 17 Julai 2014 amewashukuru viongozi wa nchi za AMECEA kwa kukuza
na kuendeleza uhuru wa kuabudu miongoni mwa wananchi wao, kielelezo kwamba, wote ni
Familia ya Mungu, licha ya tofauti zao za kidini, kijamii, kisiasa na kitamaduni.
Wajumbe
wa AMECEA huku wakiongozwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya kumi na nane ya mkutano
wake mkuu, wanapenda kujielekeza zaidi katika kuwatangazia watu wa mataifa Habari
Njema ya Wokovu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kukumbatia na
kimwilisha tunu msingi za Kiinjili, zilizohubiriwa na Yesu Kristo mwenyewe. Waamini
kwa upande wao, wanahamasishwa kuwa kweli ni mashahidi wa imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake, kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika medani mbali
mbali za maisha, ili kuyatakatifuza malimwengu.
Askofu mkuu Ziyaye anasema,
mkutano mkuu wa AMECEA utaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika masuala ya Uinjilishaji,
toba na wongofu wa ndani pamoja na uhsuhuda wa imani. AMECEA inaishukuru Serikali
ya Malawi kwa mapokezi na ukarimu ambao wamewaonjesha wajumbe wa mkutano mkuu wa AMECEA
pamoja na kuzishukuru Serikali husika kwa kuhakikisha kwamba, zinaendeleza na kudumisha
uhuru wa kuabudu na hivyo kuwawezesha Maaskofu wa AMECEA kutekeleza wajibu wao wa
kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ufanisi na tija.
Maaskofu
wa AMECEA wanasikitika kwa nchi zile ambazo uhuru wa kidini haukuheshimiwa wala kuthaminiwa;
wanaonesha mshikamano wao wa dhati na Wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wanakabiliana
na hali tete ya kisiasa kutokana na machafuko ya vita yanayoendelea nchini humo. AMECEA
inaombea haki, amani utulivu na upatanisho wa kitaifa sanjari na kuendeleza mshikamano
wa kimataifa na Kanisa la Kiulimwengu.