2014-07-17 12:33:26

Tegemezeni Kanisa Barani Afrika!


Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA, yalianza rasmi hapo tarehe 16 Julai 2014 kwa mafungo yaliyoongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, aliyekazia umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Familia ya Mungu katika nchi za AMECEA.

Jioni wajumbe walitafakari kuhusu moyo, mwono, utume na tunu msingi zinazoongoza AMECEA, mada iliyowakilishwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi pamoja na Padre Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA.

Alipowasili mjini Lilongwe, Malawi, Kardinali Njue akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba, Kanisa Barani Afrika halina budi kujipanga vyema ili kuhakikisha kwamba, linajitegemea na kujiendeleza ili kuachana na kasumba ya kuendelea kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili ng'ambo, utamaduni ambao kwa sasa umepitwa na wakati.

Ni jukumu la Maaskofu Katoliki kutoka AMECEA kuwahamasisha waamini wao ili waweze kujitegemea, kwa kuwajengea uwezo mihimili mikuu ya Uinjilishaji, ili iweze kweli kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi. Mbegu ya imani iliyopandikizwa kwa sadaka kubwa ya wamissionari inapaswa kukuzwa na kudumishwa, ili kuweza kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Maadhimisho ya mikutano ya AMECEA ni fursa ya kusali, kutafakari na kushirikishana mang'amuzi na vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Lengo ni kuhakikisha kwamba, AMECEA inairithisha Familia ya Mungu tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu. Kwa namna ya pekee, amewashukuru na kuwapongeza waamini na wananchi wa Malawi kwa mapokezi makubwa waliowaonesha wajumbe wa AMECEA walipokuwa wanawasili nchini humo kwa mkutano wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.