Kuna umati mkubwa wa waamini ambao haufahamu fika mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu
maisha ya ndoa na familia. Dhamana na utume wa Kanisa ni kuwatangazia watu Habari
Njema ya Wokovu kwa kuwakirimia watu fursa ya kukutana na Yesu Mkombozi wa dunia,
ili aweze kuwakirimia utimilifu wa maisha.
Yesu Kristo
anaendelea kuokoa Familia kwa njia ya Kanisa, kumbe, Kanisa katika mapambazuko ya
Millenia ya tatu ya Ukristo linachangamotishwa kutangaza kuhusu ukuu na utakatifu
wa maisha, urithi mkubwa uliochwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake
wa kichungaji, Familiaris Consortio, Uwajibikaji wa Familia ya Kikristo. Ni wajibu
kwa waamini kuwashirikisha jirani zao Injili ya Furaha.
Kanisa litaendelea
kulinda, kutetea na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa na familia, kwani familia
ni kitovu cha ustawi na maendeleo ya mwanadamu. Hapa kuna haja ya kuwafundisha watu
Katekesi juu ya upendo wa binadamu!