Mikakati ya kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACERAC, limehitimisha
mkutano wake mkuu ulioanza huko Brazzaville, Congo kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 13
Julai 2014 kwa kupitisha maazimio ishirini na matatu yatakayofanyiwa kazi na Familia
ya Mungu Afrika ya Kati, katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha misingi
ya Familia inayojikita katika mahusiano ya kudumu kati ya Bwana na Bibi.
Maaskofu wanasema,
Familia inakabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia sanjari na mabadiliko msingi katika maisha ya kijamii, kitamaduni
na kiuchumi; mambo yanayochangia kushamiri kwa ubinafsi, ubabe na anasa. Maaskofu
wanabainisha kwamba, hivi ni vishawishi ambavyo kimsingi vinasigana sana na tunu msingi
za maisha ya kifamilia kadiri ya mapokeo na tamaduni njema za Kiafrika; yaani ile
hali ya mtu kujitosa kisawasawa katika upendo!
Maaskofu wanakazia umuhimu wa
kufanya maandalizi ya kina kwa wanandoa watarajiwa, ili kuweza kukabiliana na changamoto
za maisha ya ndoa na familia, jambo ambalo linahitaji mikakati makini ya kichungaji
kuhusu utume wa familia. Maaskofu wanawataka waamini waliopewa dhamana katika tume
ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia kuhakikisha kwamba, zinatekeleza dhamana
na wajibu wake bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia Barani
Afrika.
Hapa mihimili ya Uinjilishaji yaani: Mapadre, Watawa na Makatekista,
wanapaswa kufundwa barabara, ili waweze kuimarisha na kuendeleza mafundisho ya Kanisa
kuhusu ndoa na familia. Wanandoa wapya wasindikizwe katika safari ya maisha yao ya
unyumba hatua kwa hatua, kwa kutambua kwamba, maisha ya unyumba si maji kwa glasi
yataka moyo kweli kweli! Wanandoa wafundishwe kuhusu utu na heshima ya binadamu, wajitambue
na kujitahidi kufahamiana kikamilifu, ili kusaidiana katika hija ya maisha ya ndoa
na familia.
Wanandoa wafundishwe tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, ili kupamba maisha yao ya ndoa kwa manukato ya tunu
msingi za Kikristo. Wanandoa wahamasishwe kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno
la Mungu katika uhalisia wa maisha; wajifunze kanuni maadili na maisha ya imani, ambayo
kimsingi yanachambuliwa kwa kina na mapana katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki
na Muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Maaskofu wanawahimiza wazazi na
walezi kujitaabisha katika kuwapatia watoto wao elimu na malezi bora ya maisha ya
Kikristo, kimaadili na kitamaduni kwa kutambua kwamba, familia ni shule ya kwanza
ya imani, maadili na utu wema. Hapa ni mahali ambapo watoto wanajifunza kujiheshimu
na kuheshimiana. Vijana wafundwe kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika maisha ya
kijamii na kikanisa; kwa kupenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, ili kutumia vyema
nguvu walizojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao na Jamii
inayowazunguka.
Familia za Kikristo zinahamasishwa kutolea ushuhuda wa maisha
yao kwa njia ya imani tendaji kama njia ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
Uinjilishaji Mpya. Wanafamilia washiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kisiasa
na kiuchumi, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya utakatifu wa maisha.
Maaskofu
Katoliki Afrika ya Kati wanawakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo yanasimikwa
katika nguzo kuu nne yaani: Neno la Mungu, Maisha ya Kisakaramenti, hasa Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho, Sala binafsi pamoja na Sala za Kifamilia.
Wanandoa wajenge utamaduni wa mawasiliano yanajikita katika ukweli, uwazi, amani na
upendo katika familia. Wajenge utamaduni wa kufanya tathmini ya maisha yao mara kwa
mara kwa kuona wapi walipopiga hatua na wapi ambapo kama familia wametindikiwa ili
waweze kuwa na ujasiri wa kuomba “divai” kwa Yesu kupitia kwa Bikira Maria. Hapa lengo
ni kujenga na kukuza utamaduni wa wongofu wa ndani, toba na msamaha katika maisha
ya waamini.
Maaskofu wanaendelea kuhimiza umuhimu wa familia za Kikristo kuheshimiana,
kupendana na kusaidiana; kwa kuheshimu na kuthamini utu na heshima ya wanawake kwani
hata wao wana mchango mkubwa. Hii ni changamoto ya kuondokana na mfumo dume unaotaka
kuwakandamiza na kuwanyanyasa wanawake na wasichana; hizi ni mila, desturi na tamaduni
ambazo zimepitwa na wakati.
Bado kuna changamoto kubwa katika kukuza na kuendeleza
ndoa mseto, hapa wanandoa hawa wanapaswa kusaidiwa kikamilifu katika kutoa malezi
na majiundo makini kwa watoto wao. Tatizo kubwa wanakiri Maaskofu ni misimamo mikali
ya kiimani inayoendelea kujengeka kwa kasi kubwa Barani Afrika.
Maaskofu wanawaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuachana na mila na desturi zinazoendekeza
uchawi na imani za kishirikina kwani mambo haya ni kati ya sababu kubwa zinazopelekea
uvunjifu wa misingi ya haki na amani, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kwa maneno
machache ni mila na desturi zinazoendeleza utamaduni wa kifo! Waamini wajifunze na
wawe waadilifu katika kutumia njia za mawasiliano ya kijamii, kwa ajili ya kujenga
na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na wala si kubomoa maadili na
utu wema. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya kati, ACERAC linahimiza
mikakati ya kichungaji inayojikita katika upendo na mshikamano kwa ajili ya kuzisaidia
familia ambazo zinajaribiwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa; kusimama
kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi pamoja na kuanza mchakato wa kuandika Mwongozo
wa wa Katekesi kuhusu Familia, itakayodumu kwa muda wa miaka mitatu. Matatizo na changamoto
zinazoendelea kuiandama taasisi ya familia, iwe ni fursa ya kushirikiana kikamilifu
na Roho Mtakatifu katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya!
Imehaririwa na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.