Chakarikeni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika!
Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki
hivi karibuni akichangia mada kwenye kongamano la kimataifa lililokuwa limeandaliwa
na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika na Madagascar SECAM kwa kuongozwa
na kauli mbiu “Kanisa Barani Afrika: kutoka Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hadi mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo: mchango wa Papa Yohane XXIII na Yohane Paulo II.”
anasema umefika wakati kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kujishughulisha na ustawi
na maendeleo yake mwenyewe kwa kuangalia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Umefika wakati
kwa wananchi barani Afrika kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na changamoto
zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na
teknolojia, ili kujipatia maendeleo ya kweli. Kwa njia hii Bara la Afrika litaweza
kutoka kifua mbele kulinda na kudumisha utu na heshima yake kwa kuwajibika barabara.
Bara la Afrika lisipoibua sera na mikakati bora ya maendeleo na ustawi wa
watu wake, litaendelea kudharauriwa na kunyanyaswa na mataifa yanayotoa misaada kwa
Bara la Afrika. Kwa sasa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, inaonekana
kana kwamba, nchi wahisani zimechoka kuendelea kubeba “zigo” la misaada kwa Bara la
Afrika. Hii ndiyo hali halisi inayojionesha kwa sasa kwani mwenye macho haambiwi atazame
mwenyewe!
Kardinali Robert Sarah ambaye aliwahi kuwa ni Rais wa kwanza wa SECAM
amewataka Waafrika ndani na nje ya Bara la Afrika kujielekeza zaidi na zaidi katika
kutafuta ujuzi na maarifa; rasilimali watu, fedha na vitu kwa ajili ya kuendeleza
Bara la Afrika, jambo linalohitaji moyo wa uzalendo, upendo na mshikamano badala ya
watu kujikita katika ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yameendelea
kulitumbukiza Bara la Afrika katika mkwamo wa maendeleo. Dhana ya Bara la Afrika kuendelea
kutegemea misaada kutoka ng’ambo imepitwa na wakati, sasa Afrika inapaswa kuwajibika
kwa ajili ya maendeleo yake.
Kardinali Sarah anasema, hadi pale Familia ya
Mungu Barani Afrika itakapokuwa na uchungu pamoja na usongo wa maendeleo yake, hapo
Afrika itaweza kucharuka kwa maendeleo. Bara la Afrika linahitaji miundo mbinu itakayojikita
katika masuala ya watu na tamaduni pamoja na imani zao. Kuna haja ya kujenga mfumo
wa maendeleo endelevu unaowajibisha na kujenga umoja na udugu pamoja na kuimarisha
uchumi unaosimikwa katika haki inayoshughulikia mafao ya wengi, kuliko hali ya sasa
rasilimali na uchumi ni kwa ajili ya watu wachache, lakini “akina yakhe pangu pakavu
weka mchuzi” wanaendelea kuogelea katika umaskini wa hali na kipato!
Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, maadhimisho ya Sinodi
mbili za Maaskofu wa Afrika zimeleta mwamko mpya kwa maisha na ustawi na maendeleo
ya Familia ya Mungu Barani Afrika. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Kanisa Barani
Afrika ni kuhakikisha kwamba, linatekeleza mashauri ya kitume yaliyotolewa na Papa
Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.
Maadhimisho ya Sinodi
ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika yaligubikwa furaha na huzuni. Kilikuwa ni kipindi
cha kuporomoka kwa sera za ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, lakini Afrika ikajikuta
inatumbukia katika majonzi makubwa kutokana na mauaji ya kimbari yaliyokuwa yanatendeka
nchini Rwanda. Kwa sasa Bara la Afrika linahitaji anasema Kardinali Peter Turkson
kujielekeza zaidi katika misingi ya haki, amani na upatanisho kutoka ndani na nje
ya Bara la Afrika.
Kwa upande wake Professa Albert Tevoedjre, Rais wa Mfuko
wa Kardinali Bernadin Gantin, nchini Benin anasema, dunia inaweza kuokolewa kutoka
kwenye mahangamizi na utepetevu wa misingi ya maadili na utu wema kwa kukumbatia na
kuenzi tunu msingi za maisha bora ya kifamilia. Jambo hili linawezekana ikiwa kama
familia zinazingatia misingi ya maadili na utu wema.
Bara la Afrika linaendelea
kushuhudia kumong’onyoka kwa maadili na msingi bora ya maisha ya familia na ndoa,
Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kukataa mielekeo inayotaka kuyumbisha tunu
bora za maisha ya ndoa na familia kwa madai ya uhuru na demokrasia.
Waamini
walei hawana budi kujengewa uwezo makini wa kupambana na mazingira yao kwa njia ya
elimu pamoja na kuwawezesha vijana kuwa na dhamiri nyofu za kuweza kupambanua mema
na mabaya badala ya mtindo wa sasa wa kuokota na kumeza kila kitu kinachooneshwa kwenye
vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kanisa Barani Afrika lazima liwekeze katika tunu
msingi za maisha ya familia na vijana, ili waamini walei waweze kuwa ni chachu ya
kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya kweli za Kiinjili, maadili na utu wema.
Kama
walivyowahi kukazia Mababa wa awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika kuna haja
ya kuwapatia wanasiasa majiundo makini yatakayowasaidia kusimamia utu na heshima ya
binadamu, mafao ya wengi na ustawi wa jamii. Mikakati hii haina budi kwenda sanjari
na majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kujikita
katika maendeleo na mafao ya wengi badala ya mwelekeo wa sasa unaowagawa wananchi
kwa misingi ya udini, jambo ambalo ni sumu kali kabisa katika kukuza na kudumisha
haki, amani na mafao ya wengi. Kinzani na migogoro ya kidini haina mashiko wala mafao
kwa ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.
Wanawake Barani Afrika wakiwezeshwa
kielimu, kiuchumi na kisiasa wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo
ya Bara la Afrika. Wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kukoleza malezi na maendeleo ya jamii husika.
Wanawake washirikishwe katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga
na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Wanawake washirikishwe
katika vikao vinavyotoa maamuzi na kwamba, mfumo dume, nyanyaso na dhuluma kwa wanawake
ni mambo ambayo hayana nafasi tena kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.
Kongamano
hili limeonesha kwa namna ya pekee mchango uliotolewa na Mtakatifu Yohane XXIII na
Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ni viongozi hawa waliothubutu
kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki kuteuwa viongozi wazalendo kutoka
Barani Afrika kama: Makardinali, Maaskofu na viongozi waandamizi ndani ya Kanisa la
Kiulimwengu, jambo ambalo lilikuwa kama ndoto kabla ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II ni viongozi wa Kanisa waliosimama
kidete katika maendeleo ya Bara la Afrika, wanapaswa kukumbukwa kwa kumwlisha mafundisho
yao katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.
Imeandaliwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.