AMECEA: shuhudieni imani yenu kwa njia ya matendo!
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Alhamisi asubuhi tarehe
17 Julai 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho
ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
Mashariki na Kati, AMECEA, yanayoongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu
na ushuhuda wa imani ya Kikristo".
Katika Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali
Njue amesema kwamba, Bara la Afrika limekirimiwa kuwa na watu wenye uchaji wa Mungu.
Yesu alimshinda Shetani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, lakini hadi leo,
Shetani bado hajasilimu amri kwamba, alishindwa kwa goli la kisigino na anaendelea
bado kuwasakama waamini na watu wenye mapenzi mema, ili kujiunga katika utawala wake.
Kardinali Njue amewapongeza Wamissionari waliojisadaka kwa ajili ya kuwatangazia
watu wa Afrika Habari Njema ya Wokovu, changamoto kwa Wakristo kuendelea kuiboresha
imani yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wa maisha. Wazazi
na walezi watambue dhamana na wajibu wao wa kuwarithisha watoto imani, maadili na
utu wema. Waamini wajitaabishe kuishuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa
njia ya maisha adili.
Zaidi ya Maaskofu 200 kutoka katika Nchi za AMECEA wanashiriki
katika mkutano wa kumi na nane wa AMECEA. Wamissionari wa kwanza walijitaabisha kutangaza
Habari Njema ya Wokovu katika mazingira magumu kiasi kwamba, wengi wao walifariki
dunia wakiwa na umri mdogo na hadi leo hii kuna makaburi yanayoonesha ushuhuda wa
majitoleo yao, lengo lilikuwa ni kuwashirikisha wananchi wa Bara la Afrika imani na
maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wamissionari hawa walikuwa
kweli waaminifu kwa Injili ya Kristo.
Kardinali Njue anawataka waamini Barani
Afrika kusafisha dhamiri zao kwa kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake katika
medani mbali mbali za maisha kwa kutambua kwamba, wasipokuwa makini na jasiri wanaweza
kumezwa na malimwengu ambayo yanaendelea kulisakama Bara la Afrika. Rushwa, ufisadi
na wizi wa mali ya umma pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu ni kati ya majanga
ya kitaifa yanayoendelea kulisonga Bara la Afrika, kiasi cha kudhohofisha sera na
mikakati ya kupambana na baa la umaskini, ujinga na maradhi Barani Afrika.
Maaskofu
wa AMECEA wanasema, wanataka kuwahakikishia waamini wao kwamba, wanapania kuwahudumia
kama wachungaji wema na watakatifu. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kusali kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa
AMECEA unaoendelea mjini Lilongwe, Malawi.
Katika Ibada hii ya Misa Takatifu
Askofu mkuu Tarcisius Ziyaye, Mwenyekiti wa AMECEA alikabidhiwa Pallio Takatifu iliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Siku kuu ya Watakatifu
Petro na Paulo, miamba wa imani, hapo tarehe 29 Juni 2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Askofu mkuu Ziyaye ni kati ya Maaskofu wakuu watatu ambao hawakubahatika
kuhudhuria na kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu.
Ibada ya Misa Takatifu
imehudhuriwa na waamini pamoja na viongozi wakuu wa Serikali ya Malawi na hasa wakati
huu wanapoendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa Jubilee ya miaka
50 tangu walipojipatia uhuru wao. Sekretarieti ya AMECEA inawapongeza waamini na
wananchi wa Malawi kwa ujumla wao kwa kufanikisha Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi
na nane wa AMECEA. Serikali ya Malawi inashirikiana kwa karibu sana na Kanisa ili
kufanikisha maadhimisho haya.