2014-07-16 09:28:12

Uinjilishaji Mpya!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, tarehe 16 Julai 2014 limeanza maadhimisho ya mkutano wake wa kumi na nane huko Lilongwe, Malawi kwa mafungo ya kiroho ambayo yameongozwa na Askofu Mengesteab Tesfamariam wa jimbo Katoliki la Asmara, Eritrea na tema kuu ni umoja! RealAudioMP3

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Josephat L. Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania anasema kwamba, Uinjilishaji mpya ni mchakato unaopania kupyaisha maisha ya Kikristo katika nyanja zote kwa kujikita katika ushuhuda unaoonesha imani tendaji. Kuna haja kwa Bara la Afrika kuendelea kuichambua na kuifafanua dhana hii ili iweze kueleweka vyema zaidi, kwani wengi wanadhani kwamba, Uinjilishaji Mpya ni kwa nchi za Ulaya na Marekani ambazo baada ya kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu, sasa zimekengeuka, kumbe zinapaswa kutangaziwa tena Injili ya Furaha kwa ari na mwamko mkubwa zaidi.

Lakini, ieleweke kwamba, Uinjilishaji Mpya unawagusa Wakristo wote, kwani wanapaswa kuendelea kumtambua, kumkiri na kumuunga Yesu katika mazingira yao mintarafu mabadiliko mbali mbali yanayoendelea kujitokeza katika maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili. Waamini watambue maana ya Ukristo wao katika karne ya ishirini na moja, hasa wakati huu watu wengi wanapojikuta wamebanwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknlojia.

Uinjilishaji mpya ni mwaliko kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatumia njia mpya za mawasiliano ya kijamii kwa ajili ya kuwatangazia watu wa kizazi hiki Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanampeleka na kumfikisha Yesu kati ya watu si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayojionesha katika vipaumbele vyao vya maisha. Waamini watambue mambo msingi katika maisha na Ukristo wao na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Askofu mkuu Lebulu anasema, Uinjilishaji mpya hautaweza kufua dafu, ikiwa kama hautagusa mifumo mbali mbali ya maisha ya mwanadamu na mazingira yake. Watu wajitahidi kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili pamoja na kuendelea kumshuhudia Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa watu wa nyakati hizi. Kwa njia ya mchakato huu, kweli Uinjilishaji mpya utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa na Mama Kanisa!

Imetarishwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.