2014-07-16 09:04:45

Rushwa, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya ni majanga ya kimataifa!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, akiwa nchini Mexico kuanzia tarehe 14- 15 Julai 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Enrique Pena Nieto wa Mexico pamoja na vyombo vya upashanaji habari nchini Mexico kwa kukazia dhamana na utume wa Kanisa Katoliki nchini Mexico kuwa ni kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili kuweza kujikomboa kutokana na hali hii pamoja na kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Parolin alikuwa nchini Mexico kushiriki katika semina iliyokuwa inajadili kuhusiana na mikakati ya kuratibu tatizo la wahamiaji nchini Mexico.

Kardinali Parolin anabainishwa kwamba, sera na mikakati ya kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa inalenga kwanza kabisa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kuzingatia haki zake msingi. Ameipongeza Mexico kwa mabadiliko makubwa inayofanya kwenye Miundo mbinu, Katiba, Sera na mikakati kwa ajili ya kulinda na kutetea haki msingi za wahamiaji nchini Mexico. Kardinali Parolin ameishukuru pia serikali ya Mexico kwa jitihada hizi zinazozingatia utu na heshima ya binadamu, hasa kwa wahamiaji ambao wanapata hifadhi katika vituo vyake vilivyoenea sehemu mbali mbali nchini humo. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kutekeleza dhamana yake kama Msamaria mwema.

Kardinali Parolin ameyasema yote haya wakati wa hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa niaba yake na Rais Pena Nieto wa Mexico. Akizungumza na waandishi wa habari amekumbushia kwa mara nyingine tena kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya umaskini na dhama ya uhamiaji ambayo kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto inayopaswa kushughulikiwa kwa njia ya mshikamano wa kimataifa. Utengano wa kifamilia na wimbi kubwa la watoto wanaojikuta wanalazimika kuhama nchi zao bila ya kusindikizwa na wazazi au walezi wao ni jambo linalohatarisha usalama na maisha ya watoto hawa.

Kardinali Parolin amegusia pia saratani ya rushwa, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya, majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Jambo la msingi ni vijana kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yao na kamwe wasikubali wajanja wachache wawapokonye matumaini waliyo nayo kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Pietro Parolin anasema katika ulimwengu wa utandawazi changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja na hakuna nchi inayoweza kujidai kwamba, inaweza kudhibiti majanga haya kwa nguvu na jeuri yake peke yake. Hapa kuna haja ya kuwa na mikakati pamoja na sera za pamoja kwa Bara la Amerika na katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.