Hakuna uhusiano wowote kati ya imani na matumizi ya nguvu!
Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2009- 2014, Tume ya Taalimungu
Kimataifa imefanya tafakari na upembuzi wa kina kuhusu Mwenyezi Mungu kadiri anavyofundishwa
na Kanisa. Tume ikajiuliza swali msingi kama kuna uhusiano wowote kati ya Imani kwa
Mungu mmoja na matumizi ya nguvu.
Tafakari
hii imefanyika katika makundi mbali mbali na hatimaye, ikajadiliwa kwa kina na mapana
na Tume hii katika mikutano yake mikuu na hatimaye, kufikia uamuzi ambao matokeo yake
yalipelekwa kwa Kardinali Gerhard L. Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho
Tanzu ya Kanisa na kuidhinisha kwamba, hati hii: “Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Utatu
Mtakatifu na Umoja wa binadamu: Ukristo katika Imani ya Mungu mmoja dhidi ya vitendo
vya nguvu.”
Huu ni utafiti unaohitaji kupatiwa majibu muafaka mintarafu uelewa
wa kitaalimungu kwani kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, kuna uhusiano wa karibu
kati ya Imani kwa Mungu mmoja na vita vya kidini; matukio ambayo yamekuwepo katika
historia ya mwanadamu. Huu ni uelewa potofu wa Mafundisho ya Kikristo kuhusu Imani
kwa Mungu mmoja.
Tafakari hii inaweza kufupishwa kwa kujiuliza maswali msingi;
Je, taalimungu ya Kikatoliki inaweza kujibu kwa ufasaha na kwa kiasi gani katika changamoto
za kitamaduni na kisiasa zinazotaka kuunganisha Imani kwa Mungu na mmoja na vita ya
kidini? Je, ukweli wa kiimani kuhusiana na Mungu mmoja unaweza kutambulika kuwa ni
nguzo na chemchemi ya upendo kati ya binadamu?
Majibu ya maswali haya msingi
ni tafakari ya kina inayojikita katika ushuhuda wa maisha kwa kukubaliana kimsingi
kwamba, vita ya kidini kwa kisingizio cha kutaka kueneza Imani kwa Mungu mmoja ni
mwelekeo potofu wa kidini mintarafu uelewa wa Kikristo uliofikia kilele chake kwa
njia ya ufunuo wa Yesu Kristo. Kanisa linatambua kwamba, ushuhuda wa Imani unajikita
kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani, jambo linalohitaji tafakari na
uchunguzi wa dhamiri ya mtu binafsi.
Sura ya kwanza yaWaraka wa Tume ya Taalimungu
Kimataifa inafafanua maana ya Imani kwa Mungu mmoja kama inavyoeleweka katika misingi
ya falsafa ya kisiasa kwa nyakati mamboleo. Wanatambua mabadiliko makubwa yaliyofikiwa
hadi hadi sasa: kutoka katika dhana ya ukanimungu hadi kufikia nyakati hizi ambako
kuna uelewa potofu wa Imani na siasa zinazotaka kung’oa uwepo wa Mungu katika maisha
ya mwanadamu.
Maana ya Imani kwa Mungu mmoja ni jambo muhimu sana katika utamaduni
mamboleo na kwa watu wanaoamini katika Mungu mmoja yaani: Wayahudi, Waislam na Wakristo.
Tume inafanya upembuzi yakinifu kwa kukataa katu katu matumizi ya nguvu kwa ajili
ya kuunga mkono dhana ya Imani kwa Mungu mmoja wala kukubaliana kimsingi na siasa
zinazotaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa maisha ya mwanadamu na vipaumbele
vyake. Kimsingi wanakubaliana na waamini na wale wasioamini kwamba, vita vya kidini
ni dhana potofu na iliyopitwa na wakati.
Kama Wanataalimungu wa Kikatoliki
wanatambua kwamba, Yesu kristo aliwafunulia wafuasi wake uhusiano wa upendo kati ya
Mungu na mwanadamu, jambo msingi katika ufahamu wa Imani kwa Mungu mmoja na kazi ya
ukombozi iliyotekelezwa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.
Katika
Sura ya Pili, Tume inaangalia sehemu za Maandiko Matakatifu ambazo ni ngumu kueleweka
kwa urahisi. Hizi ni sehemu ambazo ufunuo wa Mwenyezi Mungu unajionesha kwa namna
ya pekee na matumizi ya nguvu dhidi ya binadamu. Sehemu hizi zinafafanuliwa na vifungu
vingine vya Neno la Mungu kama tafsiri sahihi ya Neno la Mungu. Kwa kuwa na msingi
huu, Tume inaendelea kupembua mwelekeo wa kibinadamu na Kikristo katika kufafanua
tafsiri hii mintarafu matukio ya kihistoria.
Kwenye Sura ya Tatu, Tume inafanya
tafakari ya kina kuhusu uelewa wa Fumbo la Pasaka, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa
Kristo, kama nguzo msingi ya upatanisho kati ya mwanadamu. Kazi ya ukombozi ni muhimu
sana katika kutoa ufafanuzi wa kitaalimungu. Ufunuo unaojionesha katika tukio la maisha
ya Yesu Kristo, linalomfunulia binadamu upendo na huruma ya Mungu, unaonesha ukweli
wa mafundisho juu ya Kristo na Ukweli wa Fumbo la Utatu Mtakatifu dhidi ya vita vya
kidini.
Na katika Sura ya Nne, Wanataalimungu wa Kimataifa wanaelezea kwa kina
na mapana mawazo juu ya Mwenyezi Mungu mintarafu uelewa wa kifalsafa. Wanachambua
mawazo ya watu wasiomwamini Mungu pamoja na uelewa wa watu wasiokuwa na misimamo thabiti
ya kidini. Ufafanuzi hii unaendelea kujikita katika majadiliano ya kidini kwa kuonesha
uhusiano uliopo kati ya dini zinazoamini katika Mungu mmoja. Mwishoni wanatoa tafakari
ya kina inayojikita katika misingi ya kifalsafa na kitaalimungu kuhusu Ufunuo na uhusiano
wake kwa uelewa wa Mungu katika Mapokeo na hali ya kawaida.
Sura ya Tano na
ya Mwisho katika Hati hii kutoka Tume ya Taalimungu Kimataifa inatoa muhtasari wa
mambo msingi yanayokaziwa na Mama Kanisa katika mchakato wa ushuhuda wa upatanisho
kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu; na binadamu wao kwa wao. Ufunuo wa Kikristo unasafisha
dini, kwa kumweka mwanadamu mahali pake katika mchakato wa kutafuta maana ya maisha.
Ni jambo la maana sana ikiwa kama masuala ya kitaalimungu yataweza kufafanuliwa kadiri
ya maendeleo na historia ya ufunuo wa Mwenyezi Mungu kadiri ya ufahamu wa Kikristo.
Muhtasari huu umetarishwa na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.