2014-07-16 10:51:40

Ebola inaendelea kusababisha majanga!


Askofu mkuu Lewis Ziegler wa Jimbo kuu la Monrovia, amewataka waamini na wananchi wote wa Liberia katika ujumla wao, kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya ugonjwa wa Ebola ambao unaendelea kutishia miasha ya wananchi wengi Afrika Magharibi. Amewataka watu wote kuonesha ushirikiano wa dhati na Wizara ya Afya nchini Liberia katika mapambano ya ugonjwa wa Ebola.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO, zinaonesha kwamba, kuna wagonjwa 891 nchini Guinea, Liberia na Siera Leone. Hadi sasa wagonjwa wa Ebola 543 wamekwisha kufariki dunia. Wananchi wanaonywa kuwa makini katika Ibada za maziko kwa wagonjwa wa Ebola kwani wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu.

Wizara ya Afya nchini Liberia ili kukabiliana na ugonjwa wa Ebola iliandaa semina maalum kwa ajili ya viongozi wa kidini, ili kuwahamasisha waamini wao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Semina hii imehudhuriwa na viongozi wa kidini wapatao 67. Wamefundwa hatua muhimu katika kujihadhari na ugonjwa huu katika maeneo yao ya Ibada, Majumbani na kwenye Jumuiya na mikusanyiko ya watu. Viongozi hawa wamehamasishwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na kutoa taarifa haraka iwezekanapo wanapogundua uwepo wa dalili za Ebola katika maeneo yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.