Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa semina kuhusu wahamiaji
iliyoandaliwa kati ya Mexico na Vatican kuanzia tarehe 14 -15 Julai, 2014 anasema
kwamba, uhamiaji ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu
wa utandawazi, lakini bado haujapewa kipaumbele cha pekee na matokeo yake changamoto
hii imekuwa ikifanyiwa mipango ya dharura.
Uhamiaji ni dhana inayofumbata
matumaini na changamoto nyingi. Maelfu ya watu wanaolazimika kuzikimbia au kuzihama
nchi zao wanajikuta wakikabiliana na kifo, haki zao msingi haziheshimiwi wanajikuta
wakiwa wametengana na familia zao pamoja na kubaguliwa!
Baba Mtakatifu anasema
kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya kuhusiana na suala ya wahamiaji kwa kuondokana
na woga usiokuwa na mashiko, hali ya kutojali na kuwathamini wahamiaji, mambo yanayopelekea
utamaduni wa utandawazi usiojali wa kuguswa na mahangaiko ya wengine. Hapa kuna haja
ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kujenga ulimwengu bora zaidi
unaosimikwa katika misingi ya haki na udugu.
Baba Mtakatifu anawalika wahusika
kuangalia tatizo la watoto wanaolazimika kuzikimbia nchi zao pasi na msaada wa wazazi
au walezi wao kutokana na vita na umaskini, hili ni tatizo sugu linalojionesha kwa
namna ya pekee na wahamiaji kutoka Amerika ya Kati na Mexico kuelekea mpakani mwa
Marekani, ambako wanadhani kuna matumaini ya maisha, lakini ukweli wa mambo ni kwamba,
wanateseka bure!
Watoto hawa wanapaswa kupokelewa na kutunzwa kwa kusaidiwa
na sera makini na taarifa kuhusiana na hatari wanazoweza kukumbana nazo watoto hao
zitolewe kwa usahihi. Jambo la msingi ni kuwa na sera makini za maendeleo katika nchi
husika na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwajibika kikamilifu katika kukabiliana
na changamoto za uhamiaji.