Baraza la Maaskofu Katoliki Japan limeadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani, hapo tarehe
13 Julai 2014 kwa kukumbusha kwamba, majanga mbali mbali yanayoendelea kujitokeza
huko baharini madhara yake yanajionesha sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, kwa njia
ya bahari, binadamu wote wanajikuta kuwa ni Familia moja inayopaswa kuoneshana upendo
na mshikamano.
Katika ulimwengu wa utandawazi, haitoshi kufikiri na kutenda
katika dhana hii, bali kwenda zaidi kwa kujikita katika mshikamano wa upendo, changamoto
endelevu inayotolewa na Mama Kanisa kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Kila mtu ashirikishwe
katika mshikamano huu na kamwe hasiwepo mtu anayetengwa. Mabaharia na wavuvi wanapoondoka
majumbani mwao ili kuendelea na shughuli zao wanafutika machoni pa wengi, hata kama
wao ndio usukani muhimu katika mchakato wa uchumi na maendeleo ya binadamu.
Inasikitisha
kuona kwamba, watu hawa wanasahaulika mapema na ni watu wachache sana wanaweza kuwakumbuka
na kuwaombea katika shida na mahangaiko yao wanapokuwa kazini. Hata wakati mwingine,
inawawia watu wengi kuwapatia msaada wa hali na mali. Ikumbukwe kwamba, binadamu wote
mbele ya Mwenyezi Mungu ni Familia moja! Hii ni changamoto ya kuwakumbuka na kuwaombea
mabaharia na wavuvi ili waweze kutekeleza majukumu yao na kurudi salama salimini ili
waweze kuungana na familia zao.