Familia ya Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Hospitali
ya Agostino Gemelli imemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam na matashi mema kwa kuwatumia
ujumbe kwa njia ya video, kuelezea masikitiko yake kwa kutoweza kuhudhuria katika
kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kitivo cha Tiba
na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Uongozi
wa Hospitali ya Gemelli unamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatia moyo wagonjwa na wote
wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya tafiti na huduma kwa wagonjwa. Ni matumaini yao
kwamba, wataweza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu mapema iwezekanavyo!
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anawakumbuka wote ambao kwa sasa wameanza likizo
ya kipindi cha kiangazi, fursa makini ya kuweza kusali zaidi, kutafakari na kujipumzisha.
Hiki ni kipindi kigumu kwa wazee na wagonjwa wanaojikuta wakiwa mamebaki pweke. Lakini
kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawakumbuka wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali
ya Gemelli, ambao hapo tarehe 27 Juni 2014 wakati wa Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu alitarajiwa kuwatembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili yao,
lakini kutokana na afya yake kudorora dakika za mwisho akashindwa kutekeleza azma
ya moyo wake.
Baba Mtakatifu anasema anatambua mateso waliyoyapata wote waliokuwa
wamejitaabisha kwa ajili ya kuandaa tukio hili la kihistoria, lakini zaidi wagonjwa
waliotamani kusali pamoja naye katika Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kusalimiana
nao ana kwa ana. Anawakumbuka wafanyakazi wote wa Hospitali ya Gemelli wanaotekeleza
huduma kwa wagonjwa waliolazwa Hospitalini hapo, kuendelea kutekeleza wajibu huu kwa
kutambua kwamba, Mungu peke yake ndiye nguvu yao, changamoto ya kutambua na kuthamini
umuhimu wa zawadi ya maisha na Injili; upendo na huruma ya Mungu na wala si fedha
wala uchu wa madaraka. Hata mtu akijitaabisha kiasi gani hawezi kuongeza hata siku
moja ya maisha yake.
Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi, wanafunzi na wadau
waliotoka sehemu mbali mbali za Italia ili kuhudhuria tukio hili la kihistoria na
kwamba, anawapongeza kwa ajili ya majitoleo yao na kazi wanayoifanya Hospitalini hapo.
Anawaambia kwamba, bado anaendelea kujipanga ili aweze kutekeleza nia ya kukutana
na kuzungumza nao mapema iwezekanavyo. Jambo la msingi ambalo linapaswa kukumbukwa
ni kwamba, binadamu si mmiliki wa maisha yake na hawezi kuyatumia kadiri anavyotaka.
Watu wakubali udhaifu wa mwili na kuendelea kumtumainia Mungu kwamba, ndiye nguvu
yao!