2014-07-14 11:11:37

Sera na mikakati ya uchumi inayojali utu na heshima ya binadamu!


Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Vatican wamehitimisha semina iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "kwa ajili ya uchumi shirikishi", changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, "Evangelium gaudium". Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 12 Julai 2014 aliwatembelea na baadaye kupata pamoja nao chakula cha mchana.

Baba Mtakatifu akizungumza na wajumbe hawa amegusia mwelekeo wa uchumi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Uchumi usijali utu na heshima ya binadamu, hapo mwanadamu atanyanyasika na kudhulumiwa, huu ni uchumi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha mikakati na sera za uchumi na maendeleo endelevu. Anawashukuru wajumbe wa mkutano huu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake, ili kweli aweze kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Uchumi usiojali utu na heshima ya binadamu utakumbatia utamaduni wa kifo na matokeo yake yanajionesha kwa idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya. Wazee hawana nafasi tena katika mikakati na sera za kiuchumi kwani hawazalishi tena, lakini hata vijana walio na umri chini ya miaka ishirini na mitano hawana fursa za ajira wala hawana nafasi ya kujiendeleza na masomo. Ikiwa kama huu ndio mwelekeo wa sera na mikakati ya kiuchumi, dunia inaelekea kubaya!

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe kwa kushiriki kikamilifu katika semina hii ili kutoa mwelekeo wenye uwiano mzuri, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.