Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema rasimu ya Sera ya Diaspora iko kwenye
hatua za mwisho za maandalizi na muda si mrefu itaingizwa kwenye utaratibu wa Kiserikali
ili hatimaye, iweze kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri. Akizungumza na Watanzania
wanaoishi Uingereza kwenye mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania jijini London,
mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu alisema mchakato wa kuandaa rasimu hiyo ulihusisha
wadau wengi kwa kadri ilivyowezekana ili kupata wigo mpana wa suala zima la diaspora. “Katika
hatua za awali, mbali ya ofisi yangu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
tuliwashirikisha kwa karibu Umoja wa Wanadiaspora waliorudi Tanzania (Tanzania Diaspora
Initiative) na wanadiaspora kutoka Uingereza, Marekani, China, Oman, India na Afrika
Kusini ili kupata uzoefu wao kutokea huko waliko,”alisema na kuongeza: “Baadaye
tukawapelekea wataalamu ambao ni Profesa Samuel Wangwe wa REPOA, Profesa Joseph Semboja
wa Uongozi Institute na Profesa Faustine Kamuzora wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kila mmoja
kwa wakati wake na kuwaambia waichanechane kadri wawezavyo na kisha watupe mrejesho
wao.” Aliwataja wadau wengine muhimu waliohusishwa kwenye kuichambua rasimu hiyo
kuwa ni Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamiaji (International Organisation
for Migration –IOM) ambao wamebobea katika masuala ya wahamiaji katika nchi mbalimbali
duniani. “Kwa mtazamo wangu hii rasimu imekaa vizuri kwa sababu tumejitahidi kugusa
kila eneo ambalo kwenu lilikuwa na umuhimu wa kipekee. Sasa hivi imeshawekwa vizuri
kimfumo na inasubiri iingie katika utaratibu wa kiserikali,” alisema.