2014-07-14 09:17:23

Mwanadamu anawajibika kimaadili katika matumizi ya silaha!


Maendeleo ya teknolojia katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu yanaendelea kuchangia pia ugunduzi wa mbinu mpya za kivita kwa kutumia silaha ambazo zinajiendesha zenyewe, kiasi cha kufanya maamuzi juu ya hatima ya maisha au kifo cha binadamu. Tangu mwaka 2013 ujumbe wa Vatican umeonesha wasi wasi wake katika matumizi ya silaha aina ya “drone” kutokana na sababu za kimaadili ambazo zina athari kubwa kwa watumiaji na walengwa. RealAudioMP3

Maendeleo ya teknolojia yana faida kubwa katika ustawi wa maisha ya mwanadamu, lakini kutoa kibali kwa mashine kuamua kuhusu hatima ya maisha ya mwanadamu hapa ni kukiuka maadili! Ni kweli dunia inakabiliana na changamoto mbali mbali kuhusiana na afya, mazingira, vita na amani. Ni vyema ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajikita katika mikakati ya kuzuia matumizi ya silaha za “drone” kuliko kujutia matumizi haya kwa siku za usoni.

Matumizi ya silaha hizi mpya hayana budi kudhibitiwa na sheria za kimataifa zinazoongozwa na haki msingi za binadamu. Matumizi ya silaha za “drone” yanahitaji kwa kiasi kikubwa utu na maadili mambo ambayo kamwe hayawezi kupuuziwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa makini na mwelekeo wa sasa wa matumizi ya silaha za roboti katika vita kwani madhara yake yanaweza kuwa ni makubwa, ikilinganishwa na faida!

Ni mchango wa mawazo uliotolewa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa ziliziko mjini Geneva, wakati akishiriki kwenye mkutano wa wataalam kutoka Umoja wa Mataifa waliokuwa wanajadili kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya silaha zinazojiendesha zenyewe! Uamuzi kuhusu maisha ya binadamu hauna budi kutolewa kwa kuzingatia huruma, maadili na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda, mambo muhimu katika maamuzi ya hatima ya maisha ya mwanadamu.

Historia ya utengenezaji wa silaha duniani inaonesha kwamba, watengenezaji wa silaha hizi daima wamejihakikishia faida kubwa kijeshi na usambaji wake unaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya familia ya binadamu. Baadhi ya watu wanadai kwamba, kwa kutumia silaha zinazojiendesha zenyewe kuna punguza gharama, jambo ambalo linakubalika kabisa lakini gharama yake kwa maisha ya watu inaweza kuwa ni kubwa kuliko hata ilivyofikiriwa.

Watalaam wa masuala ya vita na wanajeshi wenyewe wanaonesha wasi wasi kwa kuamini matumizi ya silaha zinazojiendesha zenyewe na hivyo kuchukua nafasi ya askari. Mashine za kivita zinaweza kufanya kazi nzuri ya kutegua mabomu, kutafuta majeruhi, lakini kamwe haziwezi kumwondoa askari katika kudhibiti matumizi yake. Binadamu anapaswa kuwajibika kwa maamuzi anayoyafanya.








All the contents on this site are copyrighted ©.