Mahojiano na wasio amini yanalenga kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anasema, Bwana Eugenio Scalfari mmiliki
wa Gazeti la "La Republica" linalochapishwa kila siku nchini Italia hivi karibuni
alifanya mahojiano maalum na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu nyanyaso za kijinsia
dhidi ya watoto wadogo, Kanisa pamoja na Mafia, mambo ambayo yanavuta na kugusa hisia
za wasomaji wengi kwa nyakati hizi. Lakini kuna baadhi ya maneno ambayo yametumiwa
na mwandishi huyu ambayo kimsingi hayaoneshi uhalisia kwamba, yametamkwa na Baba Mtakatifu
Francisko, bali mawazo ya mwandishi mwenyewe!
Mahusiano kati ya Papa Francisko
na waamini; maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
Yesu wa Nazareti pamoja na Mapokeo ya Kanisa ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu
Francisko amejaribu kuyajibu katika mahojiano maalum na Bwana Scalfari. Anapenda kufanya
mahojiano na watu wasioamini ili kuwamegea upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na
Kanisa lake. Unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni jambo la kusikitisha
sana, kwani linawadumaza watoto katika makuzi na malezi yao, kiasi cha kushindwa kujenga
na kuimarisha utu wao.
Watoto na vijana wanapaswa kupewa elimu makini katika
maisha yao. Nyanyaso za kijinsia ni matendo ya udhalimu yanayoambatana pamoja na matumizi
haramu ya dawa za kulevya. Kanisa litaendelea kutoa mchango wake kwa kukazia umuhimu
wa elimu na majiundo makini ya binadamu. Kanisa halitawavumilia wale wanaojihusisha
na nyanyaso kwa watoto wadogo. Yesu alionesha huruma na mapendo kwa wadhambi, lakini
alikemea kwa ukali Pepo wabaya. Watu watubu na kumwongokea Mungu, ili kuachana na
tabia ambayo ni kinyume kabisa cha ubinadamu na utu wema. Waamini wajenge na kudumisha
dhamiri nyofu.
Baba Mtakatifu anakiri wazi kwamba, hafahamu kwa undani sana
dhana ya "Mafia" lakini anatambua madhara yanayosababishwa na Mafia. Anaendelea kujisomea
na kusikiliza shuhuda zinazotolewa na watu mbali mbali. Mafia ni kama ugonjwa ambao
watu wanaambukizana, kiasi kwamba, dhamiri inakufa na kwao hawaoni tena sababu ya
kuungama dhambi zao ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Watu wanaojihusisha
na vitendo vya mafia wanasaidiana na kufichiana siri. Kanisa litaendelea kupambana
na mafia kwani imejichimbia katika maisha na vipaumbele vya watu.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema anaendeleza changamoto za majadiliano ya kidini na kiekumene yaliyoanzishwa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Majadiliano ya kiekumene yanakabiliwa
na changamoto zake hasa kuhusiana na suala zima la useja! Viongozi wa Makanisa mengine
wanaoa, lakini kwa Kanisa Katoliki, useja ni sehemu ya sifa na sadaka inayopaswa kutolewa
na Makleri. Useja kwa Kanisa Katoliki ulianzishwa kunako Karne ya tano baada ya Kristo,
ni zawadi inayokabiliwa na changamoto nyingi!