2014-07-14 11:54:52

Kongamano la Watanzania wanaoishi ughaibuni kufanyika mwezi Agosti, 2014


Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania inaandaa kongamano la siku mbili litakalojadili mustakabali wa wana diaspora wa Tanzania kutoka nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na makampuni na wafanyabishara mbalimbali. Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipokutana na Watanzania wanaoishi Uingereza kwenye mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania jijini London.
Waziri Mkuu alisema kongamano hilo ambalo limepangwa kufanyika Agosti 14-15, mwaka huu, linalenga kuitambulisha rasmi diaspora ama jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni kama wadau muhimu katika kuleta maendeleo nchini Tanzania. "Lengo letu hasa ni kutaka jamii ya Watanzania ielewe kwamba tunao Watanzania walioko nje ya nchi kwa maelfu na kuna sehemu mnaweza kuchangia katika maendeleo ya nchi," alisema.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu alisema, katika kuitambua rasmi jamii ya wanadiaspora, Serikali itapenda kujua wako, ni wangapi na wanafanya nini ambacho kama Serikali itahitaji ujuzi/utaalamu wao, inaweza kuwapata wapi.
Alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Wanadiaspora waliorudi nchini waitwao Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
“Kongamano hilo litasaidia wanadiaspora kuweza kuona fursa mbalimbali zilizopo nchini, kuvutia wawekezaji wageni kuwekeza Tanzania, kukuza utalii nchini, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Diaspora pamoja na kuunganisha wawekezaji wa Tanzania na wawekezaji walioko nje ya nchi.”
Mada kuu ya kongamano hilo ni “Connect, Engage, Inform and Invest” na kaulimbiu yake ni “Nyumbani ni Nyumbani”. Aliwataka wajitokeze kwa wingi kushiriki kongamano hilo ambalo alisema limeandaliwa mahsusi kwa ajili yao na wasipojitokeza kwa wingi halitakuwa na maana.
Akifafanua zaidi kuhusu taswira nzima ya Diaspora, Waziri Mkuu alisema: "Sensa ya mwaka 2012 inaonyesha katika kaya zote zilizohesabiwa Tanzania Bara kuna mtu mmoja au zaidi ambaye yuko nje ya nchi. Hii ni sawa na asilimia 1.2. Kwa upande wa Zanzibar, hali iko tofauti sana. Wao ni mara mbili zaidi yaani kila kaya moja ina watu wawili na zaidi ambao wako nje ya nchi".
Alisema katika matokeo hayo ya sensa, ilibainika kwamba wanadiaspora wanaotoka kwenye kaya za mikoa ya Tanzania Bara wako 116,670 wakati wanatoka Zanzibar wanafikia 304,786.“Idadi ya Watanzania walioko Diaspora ni 421,456 ni karibu sawa na nusu milioni. Idadi hii si ndogo, ni kubwa. Na kama kundi hili lingetumika vizuri, fedha waliyonayo ambayo wanaituma kutoka nje, ingesaidia sana kuendeleza Taifa letu,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuwaelezea kuhusu mchakato wa katiba ulivyoenda na ulipofikia, maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu. “Kama Serikali tunajiandaa kwa lolote litakaloamuliwa na Bunge Maalum la Katiba. Kikubwa tunachoomba ni kuwa na mchakato wa amani hadi uchaguzi mkuu ufike,”aliongeza.
Aliwataka wanadiaspora waendelee kuiombea nchi ili ipate wagombea wenye kujali maendeleo ya watu kuliko kitu kingine chochote. “Endeleeni kuiombea nchi yetu ili tupate watu waadilifu, watu ambao wanajali watu wa hali ya chini na wenye kutaka maendeleo ya nchi kwanza kuliko vitu vingine (people who are for pro-poor development). “Endeleeni kuiombea nchi yetu amani, tuendelee kumuombea Rais Kikwete ili amalize kipindi chake vizuri na akabidhi kijiti kwa mwingine salama,” alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.