Kanisa la TAG, Tanzania linaadhimisha Miaka 75 ya uwepo wake!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amevipongeza vyama
vinne vikuu vya siasa nchini Tanzania ambavyo vimeanzisha majadiliano ya kutafuta
namna wajumbe waliosusia Bunge Maalum la Katiba wanavyoweza kurejea Bungeni. Aidha,
Rais Kikwete amewataka Watanzania kujiepusha na kishawishi cha kuingilia mchakato
wa Katiba Mpya kwa maneno na kutoa kauli nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na
uchochezi, jambo ambalo linawanyima utulivu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Rais
Kikwete pia amewataka viongozi wa dini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
waliosusia mchakato wa kutafuta Katiba kurudi Bungeni ili kumaliza kazi ya Kutunga
Katiba Mpya kama wanavyotarajiwa na Watanzania. Ili kuhakikisha kuwa kazi hiyo ya
Kutunga Katiba Mpya inakamilika bila wajumbe kulazimika kufanya kazi hiyo kwa haraka
kupita kiasi, Rais Kikwete ameliongezea Bunge hilo maalum siku 60 za ziada kwa mujibu
wa mamlaka ambayo anapewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais Kikwete ameyasema
hayo Jumapili, Julai 13, 2014 wakati alipohutubia mamia kwa mamia ya waamini wa Kanisa
la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, katika maadhimisho
la Kanisa hilo kutimiza miaka 75 tokea kuanzishwa nchini Tanzania.
Katika hotuba
yake ambako amezungumzia masuala mbali mbali likiwemo lile la Katiba Mpya, Rais Kikwete
amewaambia wananchi waliofurika uwanjani humo: “Bahati nzuri wiki iliyopita, wawakilishi
wa vyama vya CCM, CHADEMA,CUF na NCCR-Mageuzi wamekuwa wanakutana kwa jitihada za
Msajili wa Vyama vya Siasa. Naambiwa bado wanaendelea na mazungumzo. Napenda kutumia
nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa viongozi wa vyama hivyo kwa uamuzi wao wa kukutana
nakutafuta namna ya kusonga mbele. Tunatoa pongezi maalum kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa, Mheshimiwa Jaji Mutungi kwa kufanya uamuzi mzuri wa kuwakutanisha viongozi
hao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wao ndio walitufikisha hapa na wao ndiyo wenye
uwezo wa kutukwamua. Wao wana ufuasi mkubwa miongoni mwa Wajumbe la Bunge Maalum.”
Amesema Rais Kikwete: “Niwaombe Watanzania wenzangu tuwape nafasi viongozi wetu wazungumze
kwa utulivu. Tuache kwanza maneno maneno yatakayowachanganya. Maana siku hizi wasemaji
wamekuwa wengi na kauli zimekuwa nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na uchochezi
. Miluzi mingi humchanganya mbwa.”
Kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika
suala zima la baadhi ya watu kususia Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete amesema:
“Ombi langu kwa nyie viongozi wa dini ni kwamba tuwaombee ili warudi kukamilisha kazi
tuliyowatuma. Tuwaombee wote wafanye uamuzi wa pamoja. Sote tunataka warudi kukamilisha
shughuli kwa sababu mara ya mwisho lililobakia lilikuwa ni kupiga kura tu kuhusu kipengele
cha kwanza na cha sita cha Rasimu ya Katiba Mpya.”
Ameongeza:“Tuwaombee wawe
na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio. Wakubaliane juu ya kuendelea na kukamilisha
mchakato katika siku 60 za nyongeza kuanzia Agosti 5, mwaka huu, 2014. Tuombe kwa
nguvu zetu zote ili Mwenyezi Mungu awaongezee viongozi hao wapate mwafaka utakaoliwezesha
Taifa kupata Katiba nzuri na inayotekelezeka, katiba yenye kuleta umoja, mshikamano
na upendo, Katiba itakayodumisha amani na utulivu nchini na kuchohcea maendeleo ya
kasi zaidi.”
Akizungumzia masikitiko ya Kanisa la TAG kuhusu kukwama kwa mchakato
wa Katiba na rai ya Kanisa hilo kuwataka wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kurejea
Bungeni, Rais Kikwete amesema: “Masikitiko yenu ndiyo masikitiko yangu na ndiyo masikitiko
ya Watanzania wote. Rai yenu ndiyo rai yangu na ya Watanzania wote. Nafarijika kusikia
kuwa nanyi viongozi wa dini mkizisihi pande zote kurejea Bungeni na kumaliza tofauti
zao kwa mazungumzo ndani ya Bunge.”