Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana,
Jumapili tarehe 13 Julai 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican anasema kwamba, Yesu katika mahubiri yake, alitumia mifano na lugha iliyokuwa
inaeleweka kwa watu wa nyakati zake. Mfano wa mpanzi unafafanuliwa na Yesu mwenyewe
kwa kuelezea jinsi ambavyo mbegu iliyoanguka katika udongo inavyoweza kunyauka au
kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Yesu aliwafafanulia pia wafuasi wake maana ya
mifano aliyokuwa anatumia katika mahubiri yake. Anasema mbegu iliyopandwa karibu na
njia inaonesha wale wanaosikia Neno la Mungu lakini wanashindwa kulipokea, hivyo mwovu
anapokuja hulinyakua Neno hili lililopandwa mioyoni mwao. Ile mbegu iliyoangukia penye
miamba ni watu wanaolisikia Neno la Mungu na kulipokea kwa furaha, lakini Neno hili
halina mizizi katika maisha ya watu hawa, panapotokea shida na mahangaiko, wanapoteza
dira na mwelekeo.
Neno lililopandwa penye miiba, ni watu wanaosikiliza Neno
la Mungu lakini kutokana na kumezwa mno na malimwengu pamoja na tamaa ya mali wanashindwa
kuzaa matunda yanayokusudiwa. Mwishoni, mbegu iliyopandwa penye udongo mzuri ni wale
watu wanaosikia Neno la Mungu, wakalipokea, wakalitunza na kulielewa, kiasi cha kuzaa
matunda ajaa. Bikira Maria ni kielelezo makini cha udongo mzuri.
Baba Mtakatifu
anawakumbusha waamini kwamba, wao ni udongo ambao Yesu mwenyewe anaendelea kupandikiza
Neno na Upendo wake, hapa changamoto kwa kila mwamini ni kujiuliza, Je, hali yake
ya moyo iko namna gani kadiri ya mifano iliyotolewa na Yesu. Waamini watambue kwamba,
hata wao pia ni wapanzi, wanaopaswa kujichunguza kutoka katika undani wao, ili kutambua
ni mbegu gani ambayo inatoka mioyoni na midomoni mwao, ili kuipandikiza!
Maneno
yanaweza kuponya au kuangamiza; yanaweza kuwatia watu moyo au kuwakatisha tamaa, kumbe
jambo la msingi ni kutambua hapa si kile kinachomwingia mtu, bali hasa kile kinachotoka
moyoni mwa mtu. Bikira Maria awe ni mfano wa wale wanaolipokea Neno la Mungu na kuzaa
matunda yanayokusudiwa!