2014-07-12 09:26:45

Utume wa bahari na changamoto zake!


Waamini wanahamasishwa kuwa na ari na mwamko mpya katika mchakato wa utume wa mabaharia, kwa njia ya huduma makini, tafakari ya kina, uwajibikaji na uratibu mzuri wa shughuli za kichungaji kwa mabaharia na wavuvi, wanaohatarisha maisha yao kila kukicha. Hili ni ombi ambalo linatolewa na Waratibu wa Kanda katika Utume wa Bahari, baada ya kuhitimisha Kongamano la Utume wa Bahari hivi karibuni mjini Vatican. RealAudioMP3

Kongamano hili liliandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi. Wajumbe wanasema, pamoja na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo, wanakumbana kwa kiasi kikubwa na ukata wa fedha ili kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Mabaharia na wavuvi katika maeneo yao.

Bado hakuna ushirikiano mkubwa kati ya Maaskofu na Wafanyakazi wa Utume wa Bahari: Kikanda, Kitaifa na Kijimbo. Mawasiliano bado ni hafifu sana kiasi cha kugumisha utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Mabaharia na wavuvi. Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kutekelezwa kwa ajili ya Utume wa Bahari, lakini rasilimali ni tatizo kubwa kwa wakati huu.

Kumbe, wajumbe wanasema, kuna haja kwa Baraza kuteua baadhi ya wajumbe watakaoshiriki katika kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharimia shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa Bahari, unaokabiliana na changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambako utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani.

Pamoja na mapungufu haya, lakini wajumbe wanasema, kuna mambo mengi ambayo, wanapenda kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha Kanisa kutekeleza, hasa kwa kuwakirimia ujasiri wahudumu wa maisha ya kiroho kwa mabaharia kutekeleza wajibu na dhamana yao hata katika mazingira magumu sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja kwa Kanisa la Kiulimwengu kutoa msisitizo zaidi kwa ajili ya Utume wa Bahari katika Kanisa la Kiulimwengu.

Wajumbe wameshauri utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa kwneye Kongamano la XXIII la Utume wa Bahari lililofanyika mjini Vatican, kwa kutaka Utume wa Bahari kuwa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa mabaharia na wavuvi, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia vyombo vya mawasiliano ya kisasa pamoja na mitandao ya kijamii ili kuweza kuwatangazia Mabaharia na wavuvi Injili ya Furaha.
Kuna haja pia ya kuendelea kuboresha shughuli za uratibu wa Utume wa Bahari, ili uweze kuzaa matunda bora zaidi katika ulimwengu wa utandawazi, kwa kutumia rasilimali watu na fedha; weledi na utaalam kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbali mbali katika Utume wa Bahari.

Mwelekeo huu, unaweza kuwa ni chachu kwa Mabahari na wavuvi wenyewe kujisikia kuwa ni sehemu ya wadau wa Uinjilishaji Mpya, kwa kuwapatia msaada wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Biblia na Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwani hivi ni vitabu vyenye utajiri mkubwa katika ushuhuda wa imani tendaji.

Katika mapendekezo, wajumbe wanaliomba Baraza la Kipapa kuangalia upya mchakato wa kuwateuwa Waratibu wa Kanda, Utume wa Bahari; kwa kufafanua kazi, wajibu, dhamana na majukumu ya kila mhusika; kiasi cha rasilimali fedha na watu anachotakiwa kuwa nacho sanjari na maboresho ya mahusiano kati ya Utume wa Bahari na Mabaraza ya Maaskofu Mahalia. Wanalishukuru Baraza la Kipapa kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kuwapatia fursa ya kuweza kukutana, kujadili na kufahamiana zaidi pamoja na kuangalia changamoto zinazojitokeza katika utume wao, sehemu mbali mbali za dunia.

Wajumbe bado wanakumbuka changamoto iliyotolewa kwao na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewataka kuwa ni sauti ya mabaharia, wavuvi na familia zao, kwa kujikita zaidi na zaidi katika huduma kwa mabaharia na wavuvi. Wanashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa kuzunguka kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu hivi karibuni. Wajumbe wa Utume wa Bahari wanahamasishwa kutoka katika bandari salama za maisha yao, ili kuwaendelea mabaharia na wavuvi ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu wa mabaharia na wavuvi.








All the contents on this site are copyrighted ©.