Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya
Siku ya Utume wa Bahari, inayoadhimishwa tarehe 13 Julai 2014 anasema kwamba, kutokana
na hali pamoja na utume wao, mabaharia pamoja na wavuvi ni watu ambao hawaonekani
mara nyingi machoni pa watu, lakini ni watu muhimu sana katika kusukuma mbele gurudumu
la maendeleo. Kanisa linawaalika waamini katika maadhimisho haya kutowasahau mabaharia
millioni 1. 2 kutoka sehemu mbali mbali za dunia!
Katika historia ya maisha
ya mwanadamu, bahari imekuwa ni mahali ambapo: wasafiri, wavumbuzi na wafanyabiashara
wamekutana. Bahari imekuwa ni uwanja wa vita, huu ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa na kufutika
kwa baadhi ya mataifa katika uso wa dunia. Wafanyabiashara wengi wanaikumbuka bahari
kuwa ni mahali muafaka pa biashara, kwani sehemu kubwa ya bidhaa inatotumika duniani
inapitia baharini, kazi murua kabisa inayotekelezwa na mabaharia.
Mama Kanisa
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kwa kuthamini
bidhaa mbali mbali wanazotumia katika maisha yao ya kila siku ambazo ni kazi ya mikono
na jasho la mabaharia. Hili ni kundi ambali linakabiliana na changamoto mbali mbali
kila siku ya maisha yao. Mabaharia ni sehemu ya utume wa Bahari unaotekelezwa na Mama
Kanisa ili kuwaonjesha mabaharia huruma na upendo wa Mungu, ili hatimaye, hata wao
waweze kuwa kweli ni wahudumu wa Injili, katika maeneo yao ya kazi.
Maisha
ya mabaharia ni magumu na yanakabiliwa na hatari kila kukicha. Ni kundi ambalo ni
rahisi kabisa kupoteza maisha kutokana na nguvu asilia. Taarifa inaonesha kwamba,
zaidi ya mabaharia elfu moja walifariki dunia katika kipindi cha mwaka 2012 kutokana
na majanga asilia au kwa kugongana. Bado wanakabiliwa na tatizo na uharamia baharini
ambalo limeendelea kuwa sugu mwaka hadi mwaka; kunyimwa mishahara na wakati mwingine
kutuhumiwa kwa makosa ya jinai na kuzuiliwa bandarini kwa muda mrefu.
Hili
ni kundi ambalo linaishi katika hali ya upweke na wakati mwingi halina hata chembe
ya mapumziko; ni watu wanaokabiliwa na upweke pamoja na kukosa muda wa kuwa na familia
zao. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka tisini, Kanisa limeendelea kuwa bega kwa bega
katika huduma za shughuli za kichungaji kwa mabaharia kwa njia ya kitengo chake cha
Utume wa Bahari.
Kila mwaka kuna idadi kubwa ya mabaharia wanaoonjeshwa upendo
na ukarimu katika vituo vya Bikira Maria nyota ya bahari, hapa wanapata nafasi ya
kuwasiliana na familia zao pamoja na kupata huduma ya afya na maisha ya kiroho. Baraza
la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum
linasema kwamba, Utume wa Bahari imekuwa ni sauti inayowatetea mabaharia, kwa kusimama
kidete kuwalinda na kuwasaidia mabaharia kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa!