2014-07-11 12:11:31

Kilimo kwanza!


Leo tunaanza kusoma sura ya kumi na tatu ya Mwinjili Mateo anapotuletea mifano saba ambayo Yesu anazungumza juu ya ufalme wa Mungu. Mfano wa leo, unamgusa mkulima wa kawaida na shughuli zake za shambani. Ni mfano, unaoweza kuwafikirisha viongozi wa serikali wanaohamasiha wananchi kwa kauli mbiu nzuri za “Kilimo ni Uti wa Mgongo” au “Kilimo kwanza”.

Ni mfano unaoweza kumsaidia kila mkulima anayekipatia kipao mbele kilimo ili kufanikiwa katika mahangaiko ya kilimo hasa anapokosa pembejeo muhimu. Aidha kwa mfano huu mkulima anaweza kufarijiwa anapokosa mavuno licha ya juhudi na nguvu alizowekeza katika kilimo. Mkulima anaweza pia kufaidika kiroho katika mazingira yake ya ukulima akifanya vyema fikara juu ya mfano huu unaomhusu, kwani ni Mungu peke yake ndiye Mkulima hodari.

Mandhari ya mfano wa leo ni ufuoni mwa bahari ya Galilea: “Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari”. Ukweli ni kuwa Galilea siyo bahari bali ni ziwa tu. Hapa linaitwa bahari kwa hoja ya kiteolojia. Yaani tunakumbushwa bahari ya shamu waliyovuka wayahudi wakitoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi. Mandhari hii hapa inamwonesha Yesu, kuwa ni Musa wa Agano Jipya anayeliongoza Taifa Jipya kuelekea kwenye uhuru wa ufalme wa Mungu. “Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni akaketi.”

Fasuli hii pia ni ya kiteolojia, ambayo “makutano mengi” humaanisha ulimwengu mzima. Saikolojia ya jamii inatupa mang’amuzi kuwa daima kiongozi mpya huvuta watu wengi, kwa sababu anatoa sera mpya za matumaini yanayovuta hisia za watu. Mathalani, kiongozi mpya wa siasa anapotoa hotuba yenye sera zinazotumainisha maisha bora kwa kila raia, wasikilizaji wake wanahamasika kumsikiliza, kwani wanapoisikiliza hotuba hiyo wanaona kuwa ni neno la kweli la kuwakomboa.

Kadhalika hapa, watu wengi wanamkusanyikia Yesu ili kumsikiliza. Yesu anakaa chomboni kando ya bahari na kuwahutubia kwa mifano watu walioketi nchi kavu. Chombo kinachotajwa hapa ni mashua, yenye pia maana ya kiteolojia, yaani kanisa ambamo watu wa taifa jipya wamejipakia tayari kwa safari ya kuelekea ulimwengu huru. Kama ilivyokuwa wakati wa Noe chombo chake kilipopakia watu waliookoka toka kwenye gharika.

Katika mandhari hii yanajipambanua makundi mawili ya watu: Kundi la kwanza ni lile lililobaki nchi kavu. Watu hao wanasikiliza vizuri kabisa mifano ya Yesu, na wanapagawika na hotuba yake. Wasikilizaji hawa, wanaiona hotuba hiyo kuwa kama fumbo tu fulani, lakini hawatoi maamuzi ya kuingia katika mashua ili kujiunga na msafara wa Yesu wa kuelekea nchi ya uhuru, bali anabaki wakishikilia mambo yao ya nchi kavu. Kundi la pili ndilo hili la wafuasi walioingia kwenye mashua pamoja na Yesu. Hao ndio wale wanaoelewa na wanaokubaliana na mapendekezo mapya ya mwalimu wao Yesu na wanataka kusafiri pamoja naye kuelekea nchi huru.

Katika mfano huu wa mkulima, Yesu anaainisha aina nne za udongo ambamo mbegu humichwa. Mosi, udongo uliokomaa wa kwenye njia, pili udongo kidogo wa juu ya mwamba, tatu udongo wa penye miiba, na nne ni udongo mzuri. Ili kuelewa sababu za Yesu kutoa mfano huu hatuna budi kuelewa ishara za nyakati za matukio ya wakati wake. Ishara hizo ndiyo mandhari au mazingira aliyokuwa nayo, yaani hali halisi aliyoishuhudia ya kukosa mafanikio katika kazi aliyokuwa ameitolea jasho.

Yesu yuko Kafarnaumu ambako mwanzoni alipokelewa kwa kishindo na kwa hamasa sana, lakini polepole watu wakamshtukia hasa walipoanza kuuelewa ujumbe wa mafundisho yake unataka kuwapeleka wapi. Yesu anaiona hatari kwamba mafundisho yake yangeweza kuishia hewani bila kuzaa matunda au bila ya kuleta mapato hapa ulimwenguni. Mazingira na hali hii iliyompata Yesu, yanampata pia mkulima, baada ya kutoa jasho hapati mavuno anayotegemea.

Kadhalika katika imani hali hiyo tunaweza hata sisi leo tukakumbana nayo. Mathalani, tunaweza tukaiona imani yetu au Kanisa letu lipo katika kushindwa, lipo katika kuanguka au kuangamia; aidha tunaweza kuona kama vile watu hawafuati tena dini, au wanafuata kwa kufuata mapokeo bila kuwa na hamasa toka rohoni. Katika mazingira na hali kama hiyo unaweza ukaelewa vizuri sana maana ya mfano huu wa Yesu.

Hiyo ndiyo maana anayotaka kutuletea Yesu, yaani anataka kutufundisha kwamba mambo yanaweza kuonekana kwa nje kama vile ni kazi bure, kumbe ukweli siyo hivyo. Inabidi tu kuvuta saburi kwani nguvu ya uhai wa mbegu hiyo ni ya pekee sana na itatoa tu matunda kwa wakati wake.

Ardhi ya kwanza ilikomichwa mbegu ni barabarani: “mbegu inaanguka karibu na njia, ndege wanakuja kudonoa.” Katika ardhi hii, mbegu haichipuki kwa sababu imedonolewa na ndege. Hapo kosa siyo la mbegu na wala si la mpandaji. Yeye alifanya kazi yake vizuri na mbegu aliyoichagua ilikuwa nzuri yenye nguvu ya kuchipuka. Kwa hiyo shida ipo pahala ilipotua. Yawezekana hapo zamani wasafiri wengi walikuwa wanapita hivi wameikomaza nayo barabara ikawa kavu. Katika ardhi hiyo mbegu haiwezi kupenya na kuchipua. Kwa hiyo inabidi tukubali kwamba siyo ardhi zote ni nzuri. Ardhi aina hii inawakilisha hali halisi ya maisha ya leo.

Kwamba, kuna jinsi ya kutenda mambo kunakoweza kulinganishwa na njia ambamo watu hupita daima, na kutokana na mazoea hayo, namna hiyo imekomaa kama udogo wa barabarani. Mazoea hayo ndiyo yanayowasadikisha watu wote waweze kufanya hivyo, kuwaza hivyo, kwa vile watu wote wanashauri hivyo. Tunaweza kuziita ndizo njia wanamopita watu wote. Humo wanapita watu wenye vigezo na maamuzi yanayolingana na wanayofuata watu wote.

Hao ndiyo watu wa maadili ya siku za leo, wa maisha ya mtindo wa kisasa, hivi ni ngumu na haiwezi ikapokea mambo mapya ambayo ni mbegu ya ujumbe wa Kristu. Aina hiyo ya fikra ni ya udongo uliokomaa kama barabara, juu yake mbegu inabaki tu juu haiwezi kuchipua na ndege hufika na kudonoa kirahisi. Kadhalika njia huwakilisha tabia ya mtu asiyetulia kama vile msafiri. Watu walio barabarani maana yake wasafiri au wanatembea, kutokutulia pahala pamoja.

Kumbe, ili kulielewa vyema Neno la Mungu yadai kulitafakari kwa njia ya kutulia, ukimya, uvumilivu. Mapepe hawezi kuelewa maana ya Neno. Kwa mkulima unaaswa kutofuata mkumbo (wanamosafiri wote) wa kutoa kauli mbiu bila kutekeleza, aidha kilimo chadai kutulia. Kuhusu ndege anayetajwa kuwa adui anayedonoa mbegu hiyo, ni kwamba kwa Myahudi ndege hasa tai anatazamwa vibaya sana kwa sababu huharibu mazao mashambani.

Wayahudi wanaweza wakavibariki viumbe vyote vya Mungu lakini siyo ndege. Hata Ibrahimu alipotaka kufanya maagano na Mungu, ilibidi awafukuze ndege waliofika kumkorofisha “Hata tai walipotua juu ya mkonga, Abrahamu akawafukuza” (Mwanzo 15:11). Ndege wanawakilisha kitu chochote kile kinachozuia mahusiano na Mungu, yaani kitu kinachokorofisha kupokea au kusikiliza neno hadi linadonolewa kabla halijazama moyoni. Kwa hiyo moyo mkavu, wenye fikra mbovu, wenye chuki, ni kama hao ndege hufifisha kabisa neno, haliwezi kamwe kuchipua.

Ardhi ya pili ni ile iliyo juu ya mwamba “Nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota kwa udongo kukosa kina. Na jua lilipozuka ziliungua”. Maelezo ya Yesu yanasema kuwa jua hilo ni madhulumu. Mang’amuzi yanatufundisha kuwa, wale wanaosikiliza neno la Mungu kwa mara ya kwanza, wanahamasika sana, na pengine huo unakuwa ni ushabiki wa nje tu usiokuwa na kina.

Hapa tunakumbushwa pia kuangalia kwa jicho la imani unapoona katika ibada, kuna kuimba kwa motomoto nyimbo tamu pamoja na magitaa, kwa kucheza na kuvutia watu, yawezekana ikawa ni imani isiyo na kina na imebaki juu juu tu. Mapato yake imani hiyo hukinaisha na mwisho hunyauka. Mhamasiko wa aina hiyo ni wa moyo wa kijana kijana aliye katika mimi wala hakui na kukomaa ndani yangu.

Ardhi ya tatu ni ile yenye miiba: “Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga.” Miiba maana yake ni mahangaiko ya maisha, hasahasa madanganyo yaletwayo na mali, fedha, utajiri. Tatizo la msingi hapa siyo mali au utajiri, bali ni yale mahangaiko na madanganyo, kwa vile vitu hivyo vinapewa kipao mbele na vinaonekana kama vile ni vitu vya kwanza na vya pekee katika maisha.

Ardhi ya nne ni ya udongo mzuri: “Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia moja sitini, moja thelathini.” Hadi siku ya leo unaweza kusikika maneno ya mfano huu: “Mpanzi anatoka kwenda kupanda”: Yaani mpanzi Mungu anatembea katika barabara za ulimwengu wa leo, katika barabara za mioyo yetu. Huyo ni mkulima hodari mwenye moyo sana na anayeaminia sana mbegu yake na anaiamini sana ardhi aliyoiumba yeye mwenyewe ambayo ni mimi na wewe.

Ananistaajabisha sana huyu Mungu ndani mwangu aliyefanya kazi kubwa sana ya kupanda mbegu katika udongo wa moyo wangu lakini anaisubirisha mbegu ichipue lakini haoni chochote kwani mbegu imetua kwenye udongo uliokomaa wa moyo wangu, au kama imechipua na kuzaa amevuna mazao dhaifu kabisa. Amejaribu kumicha mbegu mara tatu, na kwangu mimi amemicha mara nyingi sana lakini hapati mazao; halafu mara moja tu inapotua kwenye udongo mzuri inazaa sana.

Kumbe, katika moyo au roho nzuri humo likipandwa neno, huzaa matunda mengi na mazuri, yaani huzaa maisha mazuri. Ndivyo inavyopendeza kuwaona watu wema na wazuri. Wale wanaoishi maisha ya kibinadamu kadiri ya Neno la Kristo. Neno la Krisou likipokewa vyema linazaa matunda mengi ya wema.

Yesu anataka kutujulisha hali halisi ya maisha hasa kwa wale wanaotangaza Injili au Neno la Mungu, wamwige yeye, na wasikate tamaa, bali watambue kwamba kuna aina nyingi za kupokea Neno la Mungu hata katika kiwango cha mtu binafsi. Aidha, inapendeza sana kumwona Yesu akiongea kwa mifano; kwani mtindo huo wa kuongea huacha maisha yazungumze yenyewe kwetu kwa njia ya kutufikirisha.

Yaani hutufundisha kuona kuwa vitu vidogo katika maisha siyo vitu vitupu “usidharau mwiba mguu utaota tende” yaani laiti sisi tungekuwa na macho ya kuangalia maisha au kuangalia vitu vidogo kama vile mbegu, chipuko, na mwendo wa mbingu, kazi za binadamu, na upendo wao. Laiti tungekuwa na jicho kama la Yesu la kuangalia mambo madogo madogo lakini kwa kina hata sisi tungeweza kusimulia kwa mifano, tungeweza kuzungumza juu ya Mungu kwa mfano na kwa ushairi kama alivyofanya Yesu.

Mungu aliye mkulima bora, mwema na mkarimu anamkirimu kila mtu mwema na mbaya bila ubaguzi. Ni vyema na muhimu kumwangalia Mungu katika mafanikio na katika kushindwa kwetu. Kwa kufanya hivyo huzaliwa furaha, uaminifu hata pale ninapokuwa mkavu kama njia, ninapokuwa tasa na nimezimika kabisa, Mungu anaendelea bado kupanda bila kuacha. Hata dhidi ya vikwazo vyote, miiba, kokoto, mawe njia kavu, yeye anaona tu kuwa ardhi hii inaweza kuotesha mbegu yake na kuchipua. Kazi kwangu kuotesha mbegu ya wema iliyopandwa ndani yangu hadi ilete matunda mengi ya wema.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.