2014-07-11 11:19:01

Jumuiya ya Kimataifa inalaani mashambulizi yanayoendelea Ukanda wa Gaza


Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni DR Olav Fykse Tveit, analaani vikali mashambulizi yanayofanywa na Israeli pamoja na Palestina kwenye Ukanda wa Gaza na hivyo kusababisha mateso na mahangaiko kwa watu wasiokuwa na hatia.

Haya ni matokeo ya kushindwa kwa majadiliano katika misingi ya haki na amani na hivyo kuendeleza chuki na uhasama kati ya Waisraeli na Wapalestina. Bila kujikita katika kanuni maadili, vita, chuki na uhasama vitaendelea kusababisha majanga kwa wananchi wengi huko Ukanda wa Gaza.

Israeli na Palestina wanapaswa kuheshimiana kwa kujikita katika masuala ya ulinzi na usalama; haki na amani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amelaani matumizi makubwa ya silaha dhidi ya raia wasiokuwa na hatia kuwa ni jambo ambalo haliwezi kukubalika na Umoja wa Mataifa.

Kila upande unapaswa kuheshimu na kuzingatia sheria za kimataifa na kwamba, umefika wakati wa kusitisha vita hii isiyokuwa na tija wala mashiko, bali ni kuendeleza mateso kwa watu wasiokuwa na hatia.







All the contents on this site are copyrighted ©.