2014-07-10 14:39:55

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka wa A Kanisa


Wapendwa taifa la kikuhani, karibuni katika tafakari yetu Dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa. Leo Nabii Isaya, Mtakatifu Paulo na Mwinjili Matayo wanatuambia kuwa Neno la Mungu likishaletwa kwetu haliachi kuzaa matunda hata kama kuna vipingamizi. Kumbe wajibu wetu ni kuvumilia na kuendelea kuliishi mpaka tufikie ukamilifu katikai maisha ya uzima wa milele. RealAudioMP3

Neno la Mungu ni ufunuo wa Mungu, kumbe si jambo la leo na kesho bali ni uzima uliofunuliwa kwetu. Neno hili lililo sauti ya Mungu kwetu halibadiliki kwa sababu ya kukutana na mazingira magumu au mepesi, bali huendelea kutimiza kazi yake ya ukombozi. Sisi tuliolipokea tuna wajibu wa kuvumilia magumu na mateso ili tuweze kurithi matunda yake.

Nabii Isaya anaagua neno hili la Mungu wakati Waisraeli wako utumwani. Wana mashaka na wanamlalamikia Mungu maana muda unapita na Mungu hatekelezi ahadi yake. Hatimaye Mungu anaibua kati yao, nabii Isaya awatie moyo akiwakumbusha kuwa ahadi za Mungu ni za milele, hazibadiliki. Anawafundisha kwa kutumia mfano wa mvua inyeshayo kuwa mara inyeshapo hairudi angani bali hurutubisha ardhi ili iweze kuzaa matunda. Kumbe ahadi ya Mungu ya kuwatoa katika utumwa wa kiroho na kimwili haitasimama kamwe na wala haibadiliki. Ndiyo kusema, neno la Mungu tulilolipokea halitarudi bure bali litazaa matunda.

Kutokana na fundisho hili tunaitwa kukumbuka kuwa kazi ya Mungu inayotendwa kwa njia yetu na hasa kazi za upendo zaweza kuwa na vipingamizi vingi lakini tusiogope. Bwana yu pamoja nasi. Tutoe mfano mmojawapo: jamaa mmoja aliwahi kuniambia hapendi kufunga ndoa kwa sababu baadhi ya waliofunga ndoa wameachana yaani wametengana! Nikasema: neema na makusudio ya Mungu hayaondolewi na shida kama hiyo kwa maana nia ya Mungu ni ya milele. Ataendelea kuwasaidia wale wote wanaojinyenyekeza na kuomba neema zake kila siku. Kumbe ndoa yadai maisha ya sala yaunganishayo mnyororo wa neema za Mungu. Kama kweli Mungu anakuita kwa wito huo atakupa neema kukuwezesha kuutimiza vema.

Mfano wa mpanzi katika injili unaoelezwa kwa picha ya mbegu zinazoanguka katika mwamba, njiani, katikati ya miiba na penye udongo tifutifu ni kielelezo cha vipingamizi katika kupokea imani na kuiishi. Ni picha ya ugumu na wepesi uliopo katika kueneza Neno la Mungu. Hata hivyo mwinjili anatutia moyo akisema kwa vyovyote vile injili ya Kristu itazaa matunda. Natumai ndugu waamini mmewahi kujikuta katika mazingira ya ugumu katika kuishi imani yenu, je mlikata tamaa? Hapana mlisonga mbele!

Mtakatifu Paulo anasema mateso na magumu ya leo si kitu ukilinganisha na faida tutakayopata tutakapomwona Mungu uso kwa uso ndiyo kurithi nchi aliyoahidiwa babu yetu Ibrahimu! Zaidi ya hilo anasema, je, njaa yaweza kututenga na upendo wa Kristu? Hapana, Kumbe tunaalikwa kuvumilia mateso na magumu mpaka mwisho mambo yatakapokamilika katika Kristu Yesu Mkombozi.

Niwatakie siku njema ya Bwana nikiwaomba kuimarika zaidi na zaidi mnapokutana na ugumu katika kutangaza injili ya Kristu katika maisha yenu. Tumsifu Yesu Kristo
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya cpps








All the contents on this site are copyrighted ©.