Baraza kuu la Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS katika mkutano wake uliofanyika
hivi karibuni huko Bruselles umeamua kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia
sasa, SIGNIS itajielekeza zaidi katika mchakato wa kuvisaidia vyombo vya habari kujikita
katika ujenzi wa utamaduni wa amani. SIGNIS inapenda kushiriki katika ujenzi wa utamaduni
wa amani sehemu mbali mbali duniani kwa kuwapatia watu habari za matumaini mintarafu
utamaduni wa dijitali.
Baraza linataka
kujielekeza zaidi katika kupambanua mikakati ya mawasiliano ili kufanya maboresho
makubwa katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Hiki ni kikao cha kwanza kufanywa
na Baraza hili chini ya Bwana Gustavo Andùjar pamoja na makamu wake wawili.
Itakumbukwa
kwamba, katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa SIGNIS Kimataifa uliofanyika mjini Roma,
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro
Parolin, katibu mkuu wa Vatican, aliwahimiza wajumbe kufanya tafakari ya kina kuhusu
nguvu ya mawasiliano ya jamii kwa njia ya picha zinazotumiwa na vyombo vya mawasiliano
ya jamii, ili kuonesha na kuwajengea watazamaji matumaini na kuwaondolea mashaka vijana
wa kizazi kipya.
Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia,
unaonekana kuwa na utamaduni, lugha na alama mpya kiasi cha kutengeneza taswira ya
jumla. Baba Mtakatifu Francisko aliwataka Wanahabari Wakatoliki kukabiliana na changamoto
za njia za mawasiliano ya kijamii, ili kuwashirikisha watu: hekima, ukweli na uzuri
wa Injili, katika lugha ambayo inaleta mguso na mashiko katika: akili na mioyo ya
watu, kwani kuna watu wengi wanaotafuta maana ya maisha yao.