2014-07-09 16:12:45

Yatimia miaka 25 tangu alipouawa Askofu Pietro Colombus,Mogadishu


Julai 9, Kanisa limefanya kumbukumbu ya kupita miaka 25, tangu yalipofanyika mauaji ya Askofu Pietro Salvatore Colombus, aliyekuwa Askofu wa Mogadishu Somalia, Mtawa wa Shirika la Mtakatifu Francis, aliyetumikia Kanisa katika nchi za Afrika kwa miaka 42, na maisha yake kukatishwa kwa mtutu wa bunduki hapo Julai 9, 1989. Aliuawa kwa kupigwa risasi iliyo penya moyo wake akiwa nje ya Kanisa Kuu la Mogadishu na wauaji wasiojulikana.

Kwa ajili ya kumbukumbu hii, Askofu Giorgio Bertin, Askofu wa Djibout, ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume wa Mogadishu, Jumatano hii majira ya jioni, ataongoza Ibada ya Misa, katika mji wake wa asili wa Carate Brianza, katika Jimbo Kuu la Milan.


Hayati Askofu Colombus Mfranciscan, ambaye hakuachana na joho lake la kifranciscan na tarawanda miguuni, anakumbukwa kwa unyenyekevu wake wa kichungaji, upole na ukarimu. Aliuawa akiwa na umri wa miaka miaka 67, mauaji yanayo endelea kuwa kitendawili hadi leo hii. Mazishi yake yalifanyika katika hali ya faragha yakihudhuriwa na watu wachache tu, kutokana na hali ya usalama ilivyokuwa kwa wakati huo. .

Kuna hisi za mauaji hayo, kuandaliwa na Waislamu wenye msimamo mkali, ingawa hakuna aliyekwisha dai kuhusika .
Kutokana na ukosefu wa Usalama Mogadishu, mpaka sasa, hakuna Mjumbe wa Papa Mogadishu, ila kuna msimamizi wa Kitume Askofu Giorgio Bertin, wa JImbo la Djibout, ambaye ameeleza kwamba, kwa jinsi ilivyo hata kwa wakati huu, haiwezekani kufungua ofisi za kudumu za uwakilishi wa Jimbo la Papa Mogadishu. Lakini ni wazi kwamba, tokea Djibout , wanaweza kufanya kazi za uwakilishi na wana uhusiano mzuri na serikali ya somalia, ambayo mara kwa mara, hutamka wazi wazi kwao kwamba, iwapo watajiondoa, serikali hiyo, itaishia kuwa kafara katika mikono ya watu wachache wababe wa Kiislamu.

Na kwamba hata baada ya kupita kipindi cha miaka 25 tangu kutokea mauaji ya Askofu Colombus, bado kuna mabadiliko kidogo sana katika utulivu wa kitaifa. Mwaka hadi mwaka , ghasia za mauaji na machafuko zinaendelea kuwepo zikifanywa na wababe wachache wa Kiislamu wanaotaka kuiamurisha serikali kama wanavyopenda wao iwe.

Na hii ni sababu kubwa inayozuia Kanisa, kutenda zaidi hata katika utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Somalia, hata katika maeneo ya vijijini kwa , wakulima na wafugaji. Shughuli hizi zote za kiuchumi, ni wazi zimesimama kutokana na ukosefu wa usalama na ukosefu wa taasisi za serikali.







All the contents on this site are copyrighted ©.