Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao! Ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Siku ya Usalama
Barabarani Kitaifa nchini Hispania, iliyoadhimishwa Jumapili iliyopita, tarehe 6 Julai
2014 kwa kuwataka waamini na wananchi wa Hispania kuwa makini katika matumizi ya barabara
pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee kwa watu wanaokutana nao kila siku ya maisha
yao wanapokuwa barabarani!
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika ujumbe
wake kwa maadhimisho ya Siku hii wanasema kwamba, kuna haja ya kuwa na mwelekeo chanya
unaojikita katika: upendo, ukarimu, majadiliano, hali ya kusikilizana na kuheshimiana
pamoja na kusaidiana pale inapowezekana badala ya kuwa na mwelekeo potofu, unaoonesha
jeuri, kiburi na malumbano yasiyo na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya
mtu: kiroho na kimwili.
Maaskofu wanawahamasisha waamini na wananchi katika
ujumla wao kuonesha upendo na mshikamano na watu wanaokutana nao katika hija ya maisha
yao ya kila siku, kwani kila mtu anaweza kuwa kweli ni msaada kwa jirani yake kama
ilivyotokea kwa Wafuasi wa Emmau walipokutana na kuanza kuandamana na Yesu, hatimaye,
wakamtambua katika kuumega Mkate! Tangu wakati ule wakabadilika na kuwa watu wapya
zaidi!
Maaskofu Katoliki Hispania wanawaalika waamini kutoa nafasi kwa Yesu
ili aweze kuandamana nao katika hija ya maisha yao, kwani Yesu ni Bwana, Mwalimu na
Rafiki. Ikiwa kama kweli waamini na wananchi wa Hispania watamwachia Yesu nafasi katika
maisha yao ili aweze kuwaongoza hata ajali barabarani zinaweza kupungua kwa kuwajali
zaidi watumiaji wote wa barabara.
Maaskofu kwa kushirikiana na Serikali ya
Hispania wamekuwa wakiendesha kampeni ya usalama barabarani kiasi kwamba idadi ya
vifo vinavyotokana na ajali barabarani vimepungua na kufikia watu 1, 128 katika kipindi
cha mwaka 2013. Hiki ni kiwango kidogo kabisa cha vifo vinavyotokana na ajali barabarani
tangu mwaka 1960. Watu wakiamua kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani kuna
uwezekano kabisa wa kuokoa maisha ya watu.
Watumiaji wa barabara wanakumbushwa
kwamba, maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu wasiridhike na
mafanikio haya, bali walenge zaidi kujieousha na ajali barabarani. Watumiaji wa barabara
wawe makini na wawajibike kwa maisha yao binafsi na yale ya watumiaji wengine wa barabara!