Askofu Evaristo Changula wa Jimbo Katoliki Mbeya, hivi karibuni ametabaruku Kanisa
na kuzindua Parokia Mpya ya Mtakatifu Yohane Paulo II, iliyoko eneo la Ilomba, Jimbo
Katoliki la Mbeya kwa kuitaka Familia ya Mungu Jimboni humo kuchuchumilia utakatifu
na ushuhuda wa maisha adili. Pale wanapojikuta wameelemewa na dhambi pamoja na mapungufu
yao ya kibinadamu, wakimbilie huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za
Kanisa.
Askofu Chengula amewataka waamini kuwasaidia na kuwaombea Mapadre wao,
ili waweze kutekeleza vyema huduma ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa
pamoja na huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Anawataka pia wanafamilia kuwa kweli ni mfano wa kuigwa ndani ya Jamii kwa kujikita
katika maisha adili na matakatifu, huku wakisaidiana kumpeleka Kristo katika Familia
zao ambazo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala na utakatifu wa maisha.
Waamini
wa Parokia Mpya ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili Jimbo Katoliki Mbeya wanabahati
sana kuwa na Msimamizi ambaye alisimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai,
maisha na utakatifu wa ndoa na familia; ni Mtakatifu aliyekazia umuhimu wa Uinjilishaji
wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, ni Mtakatifu
aliyetamani kuona haki na amani vikitawala katika maisha ya watu sehemu mbali mbali
duniani. Hii ndiyo changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Waamini wa Parokia
Mpya ya Mtakatifu Yohane Paulo II.
Ujenzi wa Parokia hii ulikuwa unaongozwa
na kauli mbiu ni "Hadi kieleweke" na kwa hakika sasa kimeeleweka na Familia ya Mungu
imepta Parokia ambayo lengo lake kuu ni kusogeza huduma za kichungaji kwa waamini.
Mafanikio ya ujenzi wa Kanisa hili tangu hatua za awali kabisa ni kielelezo cha ukarimu
kilichooneshwa na wazee waliotoa kiwanja kunako miaka 1970 kwa ajili ya ujenzi wa
Kigango ambacho leo hii ni Parokia.
Kabla ya ujenzi wa Kigango, waamini walikuwa
wanasali darasani, baadaye wakapata chumba kilichokuwa na matumizi mchanganyiko, Jumapili
asubuhi Ibada ya Misa Takatifu, jioni wazee walikuwa wanajirusha kwa kujipongeza kwa
kinywaji baridi. Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili imefika kwa wakati muafaka
kabisa wanasema waamini kwani wakati huu kuna mwamko mkubwa sana wa kutaka kushiriki
kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa hakika kimeeleweka!