Kanisa Katoliki nchini Malawi linamshukuru Mungu kwa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka
50 ya Uhuru wa Malawi pamoja na mafanikio makubwa yaliyokwishapatikana katika kipindi
chote hiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi. Lakini bado Malawi
inapaswa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa
vinalindwa na kuendelezwa kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu inayomwajibisha binadamu!
Bado Malawi haina budi kujielekeza katika
maboresho ya huduma ya afya na elimu kwa wananchi wake. Uchaguzi mkuu uliofanyika
nchini Malawi hivi karibuni na kumpatia ushindi Professa Arthur Peter Mutharika kuwa
Rais wa Malawi ni nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu demokrasia na ukomavu
wa kisiasa nchini Malawi sanjari na ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
wa kitaifa.
Ni changamoto ambayo imetolewa na Padre George Buleya, Katibu mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya
miaka 50 ya Uhuru wa Malawi, iliyofanyika hapo tarehe 6 Julai 2014. Kanisa limetumia
fursa hii kwa ajili ya kusali na kuiombea Malawi na wananchi wake, ili waendelee kushikamana
kwa pamoja, ili kujiletea maendeleo endelevu yanayozingatia ustawi wa mtu mzima: kiroho
na kimwili.
Padre Buleya anasema, kimsingi wananchi wa Malawi ni watu wanaopenda
amani na maendeleo. Miaka hamsini iliyopita kulikuwa na ari pamoja na moyo wa uzalendo
nchini Malawi, lakini tunu hizi msingi zinaendelea kutoweka siku hadi siku. Kuna haja
ya kuendelea kuwekeza katika maboresho ya huduma msingi za elimu, afya na maendeleo
endelevu, uhakika na usalama wa chakula kwa wananchi wote wa Malawi, kama ambavyo
pia amekazia Rais Mutharika katika hotuba yake.
Malawi inapaswa pia kukabiliana
na tatizo la rushwa na ufisadi wa mali ya umma mambo ambayo katika miaka ya hivi karibuni
yameitumbukiza Serikali ya Malawi katika kashfa kubwa kiasi kwamba, baadhi ya Nchi
wahisani ziliamua kusitisha misaada yake katika bajeti ya Malawi, hali ambayo imefifisha
utoaji wa huduma msingi kwa wananchi wa Malawi.