Vyombo vya habari saidieni mchakato wa amani na utulivu
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari wakati
huu ambapo Kenya inaendelea kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi kiasi cha kutishia
amani na usalama wa wananchi, linavitaka vyombo vya habari nchini humo, kusaidia mchakato
wa ujenzi wa upatanisho, haki, amani na utulivu kati ya watu!
Maaskofu wanawataka
wananchi wote wa Kenya kuondokana na masuala yote yanayoweza kuwagawa na hivyo kudhohofisha
umoja wa kitaifa kwa kujikita katika misingi ya ukabila na siasa. Kwa sasa Kenya inakabiliwa
na changamoto ya ukosefu wa ulinzi na usalama, kinzani na misigano ya kisiasa, ukabila,
rushwa na ufisadi.
Haya ni mambo ambayo yanatishia amani, usalama, umoja na
mshikamano wa kitaifa. Wanasiasa katika ngazi mbali mbali wanapaswa kujielekeza zaidi
katika ujenzi wa mambo msingi yanayowaunganisha wananchi wote wa Kenya, kwa kujikita
katika utawala bora unaozingatia kanuni na sheria za nchi. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya umetiwa sahihi na Padre Vincent Wambugu, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya.
Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya lilikutana
na kuzungumza na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuhusu hali tete inayoendelea kujitokeza
nchini Kenya kwa sasa. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavitaka vyombo vya habari
kusaidia mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na utulivu badala ya kushabikia maandamano
na kinzani za kisiasa.