2014-07-08 07:53:12

Papa awaomba msamaha wote waliodhulumiwa kijinsia na watumishi wa Kanisa.


Kwenye homilia yake ya siku ya mapema Jumatatu, aliyoitoa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican, Papa Francisko, aliyalenga maumivu ya kina ya wale wote wanaoteswa na usaliti wa Wakatoliki, waliotenda dhambi kubwa, ya kuwanajisi watoto kingono na madhulumu mengine ya kimwili. Katika Ibada hii kulikuwa na kundi la watu sita, kafara wa madhulumu hayo, ambao awali walikutana na Papa Francisco , na kuzungumza naye katika hali ya faragha, katika jengo la Wageni la ndani ya Vatican.

Papa Francisco akiongoza Ibada hiyo , aliiangalishwa katika kuomba msamaha, na kuungana na mateso na kilio cha kafara wote, akikumbuka mfano wa huzuni ya Petro, wakati Yesu akipita katika mateso makali kabla ya kifo chake, macho yaliyo jaa machozi yalitazamana na macho ya Bwana yaliyo jaa machozi ya mateso. Papa kwa ajili ya kanisa ameomba kwa Bwana alijalie kanisa lake hisia za dhati katika huzuni na mateso ya wote waliopitishwa katika madhulumu na unyanyasaji huu wa kutisha wa madhulumu ya ngono .

Papa alisema, leo, moyo wa Kanisa unaonekana katika macho ya Yesu, macho ya watoto waliofanyiwa vitendo vya kinyama na hivyo, unatazama na kuomba neema ya kuwalilia. Kutoa kilio kwa ajili ya watoto wake, ambao ni mtima wa matumaini ya Kanisa, waliotendewa vibaya bila hatia. Na kwa kutazama kwa kina ndani ya macho ya waathirika wa unyanyasaji, Papa alisema, anajisikia katika moyo wake, huzuni kubwa , kwa unyanyasaji huu, alioita kuwa ni zaidi ya kitendo kinyama kisicho elezeka.

Na kwamba inahuzunisha zaidi , kusikia unyama huu pia unafanywa na baadhi ya watumishi wa Kanisa kama Mapadre na Maaskofu, ambao huvunja uaminifu wao na wito wao kikuhani, na kutenda dhambi hii kubwa. Kitendo hiki ni zaidi ya vitendo vya kujidharaulisha , ni sawa na ibada ya kukufuru, kwa sababu watoto hawa waliokabidhiwa kwao katika karama ya kikuhani, kuwaongoza kwa Mungu, watoto na vijana kwa udhaifu wao kimwili, wanafanywa kuwa sadaka ya sanamu ya tamaa ya mtu. Kitendo hicho ni kunajisi sura kamili ya Mungu, sura tuliyo umbwa nayo. Vitendo hivi vya udhalilishaji na unyanyasaji wa jinsia , hasa kwa watoto huacha makovu ya kudumu katika maisha yao.

Katika hali ya huzuni Papa alieleza kwa kulinganisha huzuni yake na jinsi ilivyokuwa kwa Petro, baada ya Yesu kuhojiwa kwa vitisho, pale macho ya Petro yakiwa yamejaa machozi , yalipokutana na macho ya Yesu anaye lia. Papa alisema , mawazo yake pia anayapeleka kwa watu wengi wake kwa waume, wasichana na wavulana ambo macho yao yamejaa uchungu wa madhulumu haya. Kupitia kwao, anayaona macho ya Yesu yaliyo jaa machozi, na kuomba neema hii ya kulia kwa Bwana , neema kwa Kanisa kulia na kutoa fidia kwa wanawe na binti zake, waliodhulumiwa vibaya, watu wasio na hatia. Papa alieleza na kuwashukuru kafara wa dhuluma hizi walio safiri toka mbali kwa lengo la kukutana naye.

Homilia ya Papa, iliendelea kuililia mioyo ya watoto na vijana, iliyoumizwa wakati wakitembea katika njia ya kutaka kuelewa zaidi siri ya upendo wa Mungu na ni nia ya kukua katika imani. Alisema, leo moyo wa Kanisa unaonekana katika macho ya Yesu kwa wavulana na wasichana hawa. Papa alieleza kwa uchungu na ufahamu kwamba majeraha haya ni chanzo cha maumivu ya kina ambayo hata huvunja hisia za kiroho, na hata kukata tamaa. Wengi wa wale ambao wameteseka kwa njia hii pia hutafuta kupata msaada wa faraja katika njia ya madawa ya kulevya. Papa alionyesha kutambua kwamba, wengi waliopita katika uzoefu na wa madhulumu haya , pia huwa na matatizo katika mahusiano muhimu kama wazazi, mume na mke na watoto. Mateso katika familia huwa ni makubwa, baadhi ya familia hukabiliana hata na janga la kutisha la kifo cha mpendwa wao kujiua. Papa amezikumbuka familia hizi, na kwa moyo wa upendo wa dhati anaungana nazo katika huzuni zao.

Na kwa niaba ya Kanisa, ameomba msamaha wote kwa makosa na mapungufu ya viongozi wa Kanisa walio jihami dhidi ya makosa haya na kwa matumizi mabaya ya taarifa zilizo tolewa na wanafamilia, juu ya waathirika wa unyanyasaji. Amesema, hili lilisababisha mateso zaidi kwa upande wa wale walioathirika vibaya na kwa hatarini watoto wengine waliokuwa katika hatari za kukumbwa na dhuluma hii.

Kwa upande mwingine, aliwaomba wawe na ujasiri wa kusema yote juu ya giza hili la kutisha katika maisha ya Kanisa. Na kutangaza kwa wale wenye fikira za kufanya madhulumu haya kwamba, hakuna nafasi hiyo , katika huduma ya Kanisa, na kani halitavumilia madhara haya kufanyika kwa mtu yoyote awe mtoto au mtu mzima.

Papa amewataka Maaskofu wote, kufanya huduma yao ya kichungaji kwa uangalifu mkubwa ili kusaidia kuendeleza ulinzi wa watoto, na kuwa tayari kuwajibisha yeyote mwenye mwelekeo mpotofu, kaa Yesu alivyosema"yeyote mwenye kumkosesha mmoja wa wadogo hawa heri afungiwe jiwe na kutupwa baharini" .









All the contents on this site are copyrighted ©.