Serikali ya Uganda inadai kwamba, imefanya mashambulizi makubwa kwa wapiganaji wa
msituni ambao wamekuwa wakiwashambulia wananchi, Magharibi mwa Uganda. Jumapili iliyopita,
Kikundi cha Askari waliokuwa wamevalia kiraia kilivamia vituo vitatu ya Jeshi la Polisi
na Jeshi la Uganda katika Wilaya za Ntoroko, Bundibugyo na Kasese, zinazopakana na
DRC.
Idadi kamili ya watu waliofariki dunia katika tukio hili bado haijajulikana
rasmi, lakini viongozi wanasema kwamba, watu kadhaa wakiwemo askari na raia wamepoteza
maisha kutokana na mashambulizi haya na kwamba, zaidi ya watu tisini kadiri ya taarifa
za vyombo vya habari wamefariki dunia. Mapambano haya ni kati makabila mawili yanayokalia
utajiri mkubwa wa rasilimali ya nishati ya Petroli nchini Uganda.