Wakimbizi na wahamiaji wengi wanaendelea kuteseka kiasi kwamba, utu na heshima yao
kama binadamu vimewekwa rehani. Hawa ni wahanga wa utandawazi usiojali wala kuguswa
na mahangaiko pamoja na mateso ya watu wengine.
Kuna haja
kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji
wanaotafuta usalama na ubora wa maisha ughaibuni kwa kukimbia: vita, nyanyaso, madhulumu,
kinzani za kijamii, kisiasa, kidini na kikabila.
Ni watu ambao wameelemewa
na kongwa la umaskini pamoja na majanga asilia, kiasi kwamba, hawana tena matumaini
kwa kesho iliyo bora zaidi. Tarehe 8 Julai 2013, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea
Kisiwa cha Lampedusa, kilicho kusini mwa Italia, ili kuonesha mshikamano wa upendo
na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanohatarisha maisha yao wakiwa njia kutafuta nafuu
na ubora wa maisha.
Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa
la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalu, Jumapili iliyopita ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko
alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa.
Tangu wakati huo, bado kuna maelfu ya
watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kwa kufa maji na utupu Jangwani. Kumbu kumbu
hii anasema Kardinali Veglio ni kutaka kuamsha tena dhamiri ya Jumuiya ya Kimataifa
ili iweze kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaokufa
maji baharini. Watu wajiulize ni jambo gani ambalo limewagusa tangu walipoona majeneza
ya wahamiaji na wakimbizi yamejipanga Kisiwani pale!
Ili kujenga na kuimarisha
utamaduni wa upendo na mshikamano kuna haja ya kuwa na mtazamo mpya kuhusu wahamiaji
na wakimbizi, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana ili kuonjeshana
ukarimu kwa kumwangalia mkimbizi na mhamiaji kama binadamu anayepaswa kuheshimiwa
na kuthaminiwa, licha ya matatizo na changamoto anazokumbana nazo!
Hawa ni
watu wanaohatarisha maisha yao kiasi cha kutembea na kifo machoni pao. Hawa ni watu
wanaotoka katika nchi zile ambazo kuna vita, dhuluma na nyanyaso za utu na heshima
ya binadamu.
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, watu zaidi 75, 000
wametua nanga ya matumaini Kusini mwa Italia. Kufunga mipaka kwa watu kama hawa si
suluhisho ya kudumu, kwani ni kundi ambalo linaweza kuangukia katika mikono ya wafanyabiashara
ya binadamu! Upendo na mshikamano ni jambo la kupewa kipaumbele cha kwanza!