2014-07-07 08:54:55

Wajibu wako!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi chetu pendevu sana cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa neema za Mwenyezi Mungu tumejaliwa kuuona tena mwezi Julai. Kadiri ya desturi zetu katoliki, katika mwezi huu tunaiheshimu Damu Takatifu ya Yesu. RealAudioMP3
Taratibu za Kanisa letu zinatuelekeza kwamba, wajibu wa kwanza kabisa wa muamini mbatizwa ni kulinda muungano kamili na Kanisa kwa maneno na matendo. Muungano huo unadhihirika katika vifungo vya Imani, Sakramenti na kudumisha mshikamano na Uongozi wa Kanisa ambao Bwana Yesu mwenyewe alipenda kulithibitisha Kanisa lake. Pamoja na wajibu huo, Mwamini pia anawajibu na haki ya kuutafuta utakatifu katika maisha yake yote ili mwisho wa uzima akastahili kuirithi heri ya milele.
Kwa kutambua hayo, Mama Kanisa Mtakatifu, mwenye wajibu wa kutulea sisi watoto wake na kutuongoza kunako ukamilifu wa maisha yetu, daima anatupatia misaada ya kuweza kuupata huo utakatifu. Na daima anatuhimiza tutumie fursa hizo tunazopewa na Kanisa katika kujipatia utakatifu. Fursa hizo ni kama vile Neno la Mungu, Sakramenti na visakramenti, Toba, matendo ya upendo na huruma, mafundisho ya Kanisa, Ibada, sala na baraka mbalimbali. Ndiyo maana nyakati zote katika mwaka, Mama Kanisa ametuwekea kitu fulani cha kutusaidia katika safari yetu ya kumwendea Mungu.
Kwa mwangwi huo, kisha kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu katika mwezi uliyopita, mwezi huu wa saba tunaiheshimu Damu Takatifu/Damu azizi ya Mwokozi wetu Yesu Kristo. Ni damu ile ya Mwanakondoo asiye na mawaa, anayetajwa katika Kitabu cha Ufunuo asemwapo “...Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi” Uf.5:9-10.
Nyakati mbalimbali katika historia wachaji wa Mungu walianzisha Ibada na Jumuiya za waamini wenye roho ya kuiheshimu damu hiyo azizi ya mwanakondoo. Mtakatifu Luis wa Montifort alianzisha Ibada kwa Damu Takatifu na Moyo Mtakatifu wa Yesu akikaza kusema ‘Yesu pekee ni kila kitu kwetu na ni Yeye peke yake anaweza kuzima kiu za mioyo yetu’.
Mchaji mwingine (Padre Faber) anatufundisha juu ya muungano wa Ibada kwa moyo wa Yesu na kwa Damu takatifu ya Yesu akisema, ‘Damu Takatifu ya Yesu ina heshima na uzito wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni alama ya Damu Takatifu ya Yesu, na siyo ishara tu, bali ni nyumba yake, ngome yake na chemchemi yake. Hivyo (kadiri ya mchaji huyu), Ibada kwa Damu Takatifu ya Bwana Yesu ni Ibada inayofumbua mafumbo ya Moyo Mtakatifu wa Yesu’.
Na neno linasema ‘askari mmoja wapo, alimchoma ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji’. Ni damu ileile iliyomwagika kutoka katika madonda yake matukufu alipokuwa akiteswa. Ni damu hiyo hiyo ilichuruzika alipokuwa msalabani. Ni damu hiyohiyo ilitoka katika moyo wazi wa mwokozi. Damu ya Kristo ni alama pia ya uzima/uhai wa Kristo. Kumwaga damu yake ni kutoa uhai wake kwa ajili ya kutukomboa sisi. Ilimpendeza Bwana kwamba tukombolewe sio kwa Moyo wa Yesu tu, bali kwa Damu Takatifu. Damu Takatifu ya Yesu iliteuliwa tangu milele kuwa chombo cha ukombozi wetu.
Mmoja ya Wafuasi na waamini-makini wa Damu Takatifu ya Yesu, ni pamoja na Mtakatifu Gaspari, mwanzilishi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu. Mtakatifu Yohane Paulo II akitafakari Karama ya Mt. Gaspari na Shirika lake anatufundisha kwamba ‘Roho na Karama ya Mt. Gapari ni moyo wa maisha ya Kikrsisto. Damu Azizi ya Bwana Yesu daima imekuwa kitu cha mvuto wa pekee kwa watakatifu wote: ni shule ya utakatifu, shule ya haki, shule ya upendo na ni shule ya sadaka’. Mtakatifu Yohane Paulo II anaendelea kutualika tujizamishe zaidi katika fumbo hili la haki na upendo, na tulipeleke fumbo hili ulimwenguni kote.
Nasi kwa moyo wa upendo tunapeleka mwaliko wetu kwa Kanisa la nyumbani. Tukimbilie ulinzi wa Damu Takatifu ya Yesu, iliyomwagwa kwa ajili ya wokovu wetu. Tunapopambana na hila za mwovu, damu ya Kristo itukinge. Tunapoanguka katika dhambi, damu ya Kristo itutakase.
Mababa wa Mtaguso wa II wa Vatikani, wanatufundisha kwamba, kwa ubatizo wetu sisi sote tumeitwa kuwa wamisionari. Tunawajibu wa kumchukua Kristo na kumtangaza kokote duniani. Neno lake la wokovu liwafikie watu wote kwa nyakati zote. Basi kwa vile tunayo lulu hii ya Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu, kichungaji tunatumia nafasi hii kuwahamasisha waamini wote tuitikie kwa moyo wito huo wa kuwa wamisionari wa nyakati zetu. Kwa vijana wa Kiume na wa Kike, tujiunge na Shirika la Kimisionari hili ili tushiriki kazi ya Ukombozi wa ulimwengu kwa namna ya pekee zaidi. Waamini walei wanaweza kushiriki Karama na Roho ya Wamisionari hao wakiwa katika maisha yao ya kawaida, maisha ya familia (kama vile utawa wa tatu), yaani wakawa wafuasi wamisionari wa Damu Takatifu katika familia zao na katika mazingira yao ya kila siku. Waamini walei wanaweza kukamilisha Ukristo wao, kwa kuishi karama ya Mtakatifu Gaspari. Inapendeza na inafaa sana, ina mashiko katika maisha ya familia.
Daima tujiweke chini ya ulinzi wa Damu Takatifu ya Yesu tukisema “Ee Damu Takatifu, iliyomwagika kutoka katika madonda matukufu ya Mpendwa na Bwana wetu Yesu Kristo, utumwagikie, utuoshe, ututakase, utuponye, utuongoze na utukinge na kila uovu, majanga na magonjwa; utubariki na kutufanya tuwe watakatifu. Amina”.
Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.