TEC yawaomba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuachana na ubinafsi
Kwa mujibu wa Gazeti la” This Day” Askofu Tarcius Ngalelakumtwa, Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa
wiki, alisema, TEC imefadhaishwa na kuzuka kwa mabishano makali na mpasuko uliosababisha
upotoshaji wa nia iliyo kusudiwa ya kuunda Bunge Maalum la Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania.
Askofu Ngalelakumtwa, alitumia nafasi hiyo kukumbusha
kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, kwa ujasiri
wa kipekee alianzisha mchakato wa kuunda katiba mpya, na kisha aliridhia kwa furaha
, kuipokea rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini kutokana na
hali ya mvutano mkali na utengano uliojitokeza katika Bunge maalum la Katiba, Rais
wa TEC, ametoa wito kwa Watanzania, kujiuliza nini kimetokea hadi mwelekeo mzima wa
mabadiliko ya Katiba kugeuka kabisa kwa kuikejeli na kuishutumu vikali rasimu hiyo,
ambayo inatakiwa kuandika historia ya kipekee ya Bunge Maalum la Katiba. pia inashangaza
jinsi wajumbe wake walivyo sahau gharama kubwa, iliyo bebeshwa walipa kodi wakati
wakiiijadili, na sasa majadiliano hayo yanaonyesha dhahiri kutaka kuiingiza nchi
katika mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbele.
Rais wa TEC anaendelea kusema,
wakati wa uzinduzi, Rais Kikwete aliweka wazi msimamo wake kwamba rasimu ya pili ya
Katiba ilikuwa na kasoro nyingi na kusema kwamba wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kusoma
ukurasa kwa ukurasa, sentensi kwa sentensi, neno kwa neno na wakiona kuna mambo ya
kubadilisha wayabadilishe.
Kumbe tatizo liko wapi? Askofu Tarcisio Ngalelakumtwa,
ametaja maoni ya TEC katika mgogoro huu wa Katiba kwamba, ni kukosekana kwa utashi
na uwajibikaji wa kisiasa na wajumbe kutokuwa wakweli juu ya suala zima la mchakato
wa Katiba. TEC imewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwa wamoja na kufanya
kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama, ili mchakato uwezeshe upatikanaji
wa katiba mpya.“Kuandika katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama,
hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda Katiba mpya kwa kuzingatia rasimu ya pili utaweza
kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu,” alisema Rais huyo ambaye pia ni Askofu wa Jimbo
la Iringa.
Na aliwaasa kwamba , “iwapo matokeo yatakuwa yenye kuleta mema
na kuimarisha amani na utulivu Tanzania, watu wote watawashukuru na kuwasifu, lakini
kama tunda la kazi yao litakuwa la kuingiza nchi kwenye matatizo zaidi, ni kuwataabisha
wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi watu watawahukumu na kuwawajibisha kwa
kukosa umakini katika jukumu walilokabidhiwa”