2014-07-06 09:27:40

Usithubutu kubadili Katiba!


Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO, limemsihi Rais Joseph Kabila wa DRC kuheshimu Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama na kuachana kabisa na wazo la kutaka kubadili Katiba, ili kupata nafasi ya kuweza kushiriki tena katika kinyang'anyiro cha urais wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo kunako mwaka 2016.

Kutaka kung'ang'ania madarakani, kunaweza kutibua mustakabali na maendeleo ya DRC ambayo hadi sasa inaendelea kuchechemea kutokana na vita na kinzani za kijamii na kisiasa. Uchu wa mali na madaraka umepelekea wananchi wengi Barani Afrika kujikuta wanakabiliana na majanga mbali mbali ya maisha, mambo ambayo yamekwamisha mchakato wa kujiletea maendeleo endelevu hata kama nchi hizi zina utajiri na rasilimali ya kutosha ambayo ingesaidia kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Uhuru wa DRC, hivi karibuni, linaonya kwamba, wazo la kutaka kupindisha katiba linaweza kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa, changamoto ambayo imetolewa pia na wawakilishi wa Jumuiya mbali mbali za Kimataifa nchini DRC. Rais Joseph Kabila alishinda kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka 2006 na kupata tena ridhaa ya wananchi ya kuwaongoza kunako mwaka 2011 na sasa anataka kubadili Katiba ili aweze kushiriki tena katika uchaguzi wa Mwaka 2016.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali kuanza mchakato wa zoezi la kupiga kura mapema, kama sehemu ya kuwajengea wananchi uwezo wa kushiriki katika demokrasia, ustawi na maendeleo yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.