2014-07-06 07:42:50

Gerezani kuna mateso, lakini ni mahali pa matumaini kwa toba na wongofu wa ndani!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzungumza na vijana kutoka Molise na Abruzzo Jumamosi tarehe 5 Julai 2014, jioni alikwenda moja kwa moja hadi Jimboni Isernia, ili kukutana na kuzungumza na wafungwa wanaotumikia adhabu gerezani Isernia. Amemshukuru Mkuu wa Gereza kwa maneno ya matumaini, changamoto kwa wafungwa wanaotamani baada ya kumaliza adhabu zao kuanza tena maisha mapya uraiani, jambo ambalo linakumbana na changamoto nyingi. RealAudioMP3

Hii ni hija inayofanywa na wadau mbali mbali ndani na nje ya magereza; katika Jamii, lakini zaidi sana katika undani wa maisha ya mtu mwenyewe, akiongozwa na dhamiri nyofu na moyo mweupe! Baba Mtakatifu anawaambia wafungwa kwamba, hawana budi kujishughulisha kusonga mbele pasi na kukata tamaa, wakiomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii ni safari ya wote kwani kama binadamu wote hutenda dhambi, hivyo hawana budi kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mungu ambaye daima yuko tayari kusamehe.

Watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba mwema na mwingi wa huruma anawapenda daima. Wakimtafuta kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, atawapokea na kuwakirimia msamaha kwani Mwenyezi Mungu, kamwe hachoki kusamehe. Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo kauli inayoongoza hija yake ya kichungaji Mkoani Molise.

Mwenyezi Mungu anawawezesha na kuwakirimia utu wao katika ukamilifu wake na kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwasahau, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, daima wako kwenye kumbu kumbu yake. Kwa imani na matumaini haya, inawezekana kabisa kufanya hija ya maisha hatua kwa hatua, siku kwa siku na kwamba, upendo aminifu unasindikiza matumaini haya ambayo kamwe hayawezi kudanganya.

Watu wanateseka ndani na nje ya magereza, jambo la msingi ni kusafisha dhamiri ili iweze kuwa safi, kumbe mateso anayopata mwanadamu yamsaidie kuwa na matumaini kwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kuonja tena huruma na upendo wa Mungu, tayari kuanza maisha mapya uraiani.

Kwa upande wake, Barbara Lenzini, Mkuu wa Gereza la Isernia amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hawataweza kuisahau siku hii ambayo amewatembelea na kuzungumza nao Gerezani hapo. Wanakosa maneno ya kumwambia, lakini wanatoa shukrani zao za dhati kwa kuwatembelea katika eneo la mateso ambalo watu wengi wasingependa kulikumbuka wala kuzungumza juu yake. Ni eneo hai la lenye matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Siki huu iwe ni mwanzo mpya na mchakato wa mageuzi ya ndani.

Wafungwa wa gereza la Isernia wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaonjesha: fuaraha, upendo, matumaini na huruma inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu wengi wanaona gereza ni shimo la taka za kijamii, lakini hapa panapaswa kuwa ni mahali pa kumwelimisha mfungwa ili aweze kuwa ni mtu bora zaidi anapomaliza adhabu yake gerezani, kwa kugundua na kuendeleza utu na heshima yake.

Magereza yamefurika wafungwa hali inayodhalilisha utu na heshima yao. Wanasiasa badala ya kusaidia kutatua tatizo hili, kila siku wanagombana Bungeni. Umefika wakati kwa wanasiasa kuangalia kwa umakini mkubwa mfumo wa magereza nchini Italia, ili kuboresha maisha ya wafungwa kwa kuheshimu uhuru na haki msingi za binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.