Baba Mtakatifu bado anawalilia wahamiaji wanaokufa maji wakiwa njiani kwenda Ulaya!
Askofu mkuu Francesco Montenegro wa Jimbo kuu la Agrigento, Kusini mwa Italia, Jumamosi
jioni tarehe 5 Julai 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu
ya mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa kushuhuhudia
mwenyewe kwa macho yake mateso na mahangaiko ya wahamiaji waliokuwa wanakufa maji
na kiu jangwani wakati wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya.
Itakumbukwa kwamba,
hija hii ilifanywa na Baba Mtakatifu hapo tarehe 8 Julai 2013. Tangu wakati huo kuna
wahamiaji wengi wameendelea kufa maji baharini.
Baba Mtakatifu Francisko katika
ujumbe wake kwa ajili ya kumbu kumbu hii, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha
kutembelea Lampedusa, ili kuonesha mshikamano wake na wahamiaji pamoja na kusali kwa
ajili ya kuwaombea maelfu ya watu wanaokufa maji baharini, wakiwa njiani kutafuta
unafuu wa maisha pamoja na kuamsha dhamiri za watu ili waweze kuguswa na mateso ya
watu hawa.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Lampedusa
kwa upendo na mshikamano wanaouonesha kwa wahamiaji. Shukrani hizi zinawaendea pia
wananchi wote wa Italia ambao kweli wameonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wahamiaji
kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni vigumu kupokea misiba ya wahamiaji wanaokimbia
majanga ya maisha; umaskini, vita na kinzani ambazo wakati mwingine zinauhusiano wa
moja kwa moja na siasa za kimataifa.
Baba Mtakatifu anasema wakati huu anapenda
kuungana nao kiroho ili kuwalilia wahamiaji wanaoendelea kufa maji baharini pamoja
na wote wanaotupa mashada ya maua ya sala kwa ajili ya kuwakumbuka wahamiaji hawa,
wanaopaswa kushughulikiwa kikamilifu badala ya kuwageuzia kisogo, bali kwa kuwaonjesha
upendo na ukarimu, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki zao
msingi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na wala si vinginevyo!
Baba
Mtakatifu anaendelea kuzihimiza Jumuiya za Kikristo pamoja na watu wenye mapenzi mema
kuendelea kuwaonjesha upendo na mshikamano wale wote wanaohitaji bado msaada wao,
bila kudai, kuogopa, bali kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko yao. Ni matumaini
ya Baba Mtakatifu kwamba, taasisi za kimataifa zitajitahidi kuonesha ujasiri na ukarimu
kwa wakimbizi na wahamiaji, ili kupata ufumbuzi wa kudumu katika matukio haya!