Wafanyakazi: zingatieni tafiti za kisayansi na majiundo makini ya kazi!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi asubuhi tarehe 5 Julai 2014 amewasili Mkoani Molise,
Kusini mwa Italia na kupokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali, wakiongozwa na
Askofu mkuu Giancarlo Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso-Boiano.
Baadaye, Papa
amekwenda moja kwa moja kwenye Chuo Kikuu cha Campobasso na hapo amewahutubia wafanyakazi
kutoka ndani na nje ya mkoa wa Molise kwa kukazia umuhimu wa tafiti za kisayansi na
majiundo makini katika ulimwengu wa kazi, ili kujibu changamoto zinazojitokeza kutokana
na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Anasema, mwenyezi Mungu anaendelea kumshangaza
na kumchangamotisha mwanadamu kuwa na ujasiri wa kuvunjilia mbali vikwazo kwa kuonesha
kipaji cha ugunduzi kielelezo cha matumaini.
Amewapongeza vijana wanaojizatiti
katika kilimo ili kusaidia shughuli za uzalishaji kwa kutambua kwamba, si rahisi kupata
majibu muafaka na wazi yanayojikita katika ugunduzi ili kutumia kikamilifu rasilimali
inayopatikana katika eneo husika. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kweli ili ardhi
iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Amewataka wakulima kutumia vyema ardhi waliyokabidhiwa
na Mwenyezi Mungu kwani hii ni kati ya changamoto kubwa zinazomkabilia mwanadamu katika
ulimwengu mamboleo. Ardhi itumike vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu kwa
kuheshimu kazi ya uumbaji. Uharibifu wa mazingira una madhara makubwa sana kwa binadamu.
Changamoto
nyingine inayojitokeza katika ulimwengu wa wafanyakazi ni wanawake wanapaswa kufanya
kazi na wakati huo huo kutekeleza majukumu yao ya kifamilia. Huu ni ushuhuda wa kweli
unaohitaji kuwa na uwiano mzuri kati ya wajibu wa kazi na dhamana ya kifamilia, kwa
kuzingatia utu na heshima ya binadamu katika sekta ya uchumi ambamo mwanadamu anaishi.
Ni mwaliko kwa wazazi kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
familia zao kwani maendeleo ya uchumi mamboleo hayana nafasi tena kwa familia, kwani
inaonekana kana kwamba ni kupoteza muda.
Hapa kuna haja ya kuheshimu na kuthamini
Jumapili, siku ya mapumziko si tu kwa ajili ya waamini bali kwa ajili ya wafanyakazi
wote kwani hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni kanuni maadili.
Jambo
la msingi ni kuangalia mambo yale yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza pamoja
na kuendeleza kazi msingi kwani kipaumbele cha kwanza hapa ni binadamu na wala si
faida ya kiuchumi; mahusiano ya kifamilia na wala si ya kibiashara na kwa waamini
ni kujitahidi kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu pamoja na Jumuiya ya Waamini.
Umefika
wakati muafaka wa kujiuliza ikiwa kama kufanya kazi Jumapili ni kielelezo cha uhuru
wa kweli! Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kielelezo cha uhuru
wa kweli!
Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema anapenda kuungana na wafanyakazi
na wafanyabiashara kuomba kuanzishwa kwa mchakato wa "mkataba wa kazi" kama njia ya
kupambana na ukosefu wa fursa za ajira mkoani Molise, kwa kuunganisha nguvu za pamoja
ili kuokoa nafasi za kazi kwa kuwa na mkakati makini kwa kushirikiana na viongozi
wa kitaifa. Mkataba wa kazi unaoweza kusoma alama za nyakati kwa kuchangamkia fursa
zinazotolewa na sera za kitaifa na kutoka katika Jumuiya ya Ulaya.
Baba Mtakatifu
anawahimiza wafanyakazi kujizatiti katika mwelekeo huu, kwani kuna matumaini kwamba,
unaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa hata kwa mikoa mingine pia. Utu na heshima ya
binadamu; mahitaji yake msingi kwani inasikitisha kuona kwamba, mzazi anashindwa kutekeleza
wajibu wake msingi kwa kuipatia familia yake chakula kwa vile hana fursa ya ajira.
Jambo hili linasikitisha kwani linamwondolea mtu utu na heshima yake, kumbe, kuna
haja ya kufanya kazi ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu!
Baba
Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi kwa kumzawadia Picha inayoonesha "Umama", kielelezo
cha maisha na matumaini mapya. Anawashukuru kwa zawadi, lakini zaidi kwa ujumbe unaofumbatwa
katika zawadi hii ambayo imesheheni kwa matumaini.
Kwa upande wake, Professa
Gianmaria Palmieri, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Campobasso, kwa niaba ya wafanyakazi na
wakulima kutoka mkoa wa Molise, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea,
kwani hii ni sehemu ambayo imekiriwa utajiri mkubwa wa maliasili, utamaduni, mapokeo
lakini zaidi kwa rasilimali watu, watu ambao ni waaminifu, wenye kiasi na wachapakazi,
lakini kwa bahati mbaya wanaishi pembezoni mwa Jamii.
Hapa kuna changamoto
nyingi zinazoendelea kujitokeza kwani vijana wengi wanajikuta hawana nafasi za ajira
hivyo kuukimbia mkoa huu ili kujitafutia nafuu ya maisha. Ukosefu wa ajira ni tatizo
kubwa mkoani hapo na kwamba, kuna wawekezaji na wafanyabiashara wamelazimika kufunga
shughuli zao kutokana na ukata wa fedha.
Mkoa huu umebahatika kuwa na rasilimali
nyingi, zikitumika kikamilifu zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ukuaji wa
uchumi na maisha ya watu. Wafanyakazi wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia
moyo, ari na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha bila ya kukata tamaa.
Naye
Gabrieli Maglieri kijana mwenye umri wa miaka 28 amemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko
jitihada zake katika masomo, ili kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo kwa kutunza
na kuendeleza mazingira; kwa kuheshimu na kuthamini kazi inayotekelezwa na wakulima,
changamoto kwa vijana kujihusisha na shughuli za kilimo badala ya kuwaachia wazee
peke yao na kwamba haki inapaswa kutendeka!
Mama Eliza Piermarino, amemshirikisha
Baba Mtakatifu changamoto anazokabiliana nazo katika maisha yake ya kazi na wajibu
wake kama Mama wa familia nyumbani. Amezungumzia kuhusu ufanisi na changamoto kubwa
anazokabiliana nazo katika ulimwengu wa kazi. Haya ni mang'amuzi yanayowagusa wanawake
wengi wanaofanya kazi ofisini na viwandani. Ameonesha wasi wasi kwa maisha ya familia
yake kwa siku za usoni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa!