Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa kuongoza tena kwa kipindi cha miaka mitano!
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amethibitishwa
tena kuendelea na utume wake katika kipindi cha miaka mitano tena kuanzia sasa. Huu
ni uamuzi uliofanywa na Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni iliyokuwa inafanya
kikao chake mjini Geneva hapo tarehe 3 Julai 2014. Dr Tveit amepokea dhamana hii kwa
mara nyingine tena kwa moyo mkuu na shukrani.
Miaka mitano iliyopita, imekuwa
ni miaka ya neema na baraka tele kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na sasa Baraza
litaendeleza hija yake ya maisha ya kiekumene, ili kukabiliana na matatizo, changamoto
na mapungufu mbali mbali yanayoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Baraza
la Makanisa Ulimwenguni. Hii ni nafasi nyingine tena inayomwimarisha katika maisha
na utume wake kama Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema Dr. Tveit.
Taarifa
inaonesha kwamba, miaka kadhaa iliyopita, Dr. Tveit amejitahidi kuimarisha mahusiano
kati ya Makanisa duniani pamoja na kuendelea kuhamasisha Jumuiya za Kikristo kusimama
kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani. Ni matumaini ya Dr. Tveit kwamba,
ataendeleza kazi na utume wake aliouanza kwenye awamu yake ya kwanza ya uongozi wake
kama katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano
ya kiekumene miongoni mwa Makanisa Ulimwenguni.